Saturday, May 5, 2012

KIswahili kinazikwa

Watu wamenunuliwa, Kiswahili kukiua,
Ujanja wanatumia, wengine kuwahadaa,
Kumbe wao kulemaa, ndio wanakazania,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Ugiriki walikuwa, wa kwanza kwenye dunia,
Elimu kupalilia, mengi tusiyoyajua,
Hadi leo tunajua, mema yaliyozaliwa,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Ila walihadaiwa, dharau ikawajaa,
Lugha wakapuuzia, Kilatini kuingia,
Walipokujashtukia, marehemu imekuwa,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Walipokujashtukia, marehemu imekuwa,
Kimataifa yapwaya, ngumu kujaheshimiwa,
Uzito imepungua, ukimwi kuiingia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Kilatini nacho pia, siku kilipozainiwa,
Wasomi wakajitia, tajiri tu wanafaa,
Na wakubwa walokuwa, lugha hiyo kuijua,
Walipokujashtukia, marehemu imekuwa,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Masikini kuambiwa, kubwa kwao imekuwa,
Hawafai kuijua, haitowasaidia,
Kumbe imehukumiwa, kaburini kuingia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Zipo nyingi lugha pia, katika hii dunia,
Wakubwa walipopwaya, ulinzi wakaachia,
Mageni kukumbatia, madawa yakawalevya,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Na pale walipolewa, lugha zao kujifia,
Ni watumwa wamekua, inawacheka dunia,
Laiti wangelijua, haya yasingetokea,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Yatufunza historia, lugha uwezavyo kuua,
Hapa kwetu Tanzania, ndicho sasa chatokea,
Bungeni imefikia, wauangaji  waingia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Laana nawaombea, mema wasiyoitakia,
Ianze kwao kutua, na kizazi kufatia,
Kama wakija kuua, lugha yetu asilia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Masikini mwatakiwa, lugha yenu kutetea,
Kwa uchumi imejaa, si fukara nawambia,
Ila wasiojaliwa, udni wanatutia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Kiswhili mashalaa, kutawala kinafaa,
Tena sio Tanzania, hata pia na dunia,
Kiarabu kimejaa, themanini yake mia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Kiarabu kimejaa, thamania asilimia,
Kama chaweza wafaa, kwanini sisi kuvia,
Ila tumelogewa, wanyonyaji kutunywea?
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Hasira nimeitia, na kweli nawaambia,
Viongozi walokuwa, dhambi wametufanyia,
Na alam tutatia, Kiswahili waliua,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

KIONGOZI maridhia, kuenziwa Tanzania,
Lugha atakayeamua, Kiswahili kutumiwa,
Wengi wapate jaliwa, elimu kuendelea,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Wengi wapate jaliwa, elimu kuendelea,
Lugha wakifundishiwa, hadi daktari kuwa,
Ikiwa wanaridhia, nyingine watazijua,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Ikiwa wataridhia, nyingine watazijua,
Tena wawe wachagua, na sio kuamriwa,
Kiarabu kikifaa, basi wataendelea,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Kiarabu kikifaa, hiyo sawa itakuwa,
Kichina chafaa pia, maabara wataingia,
Huko watajisomea, hata pia lugha mia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Lakini kuendelea, chetu tutakitumia,
Hadi tafiti kutia, wenyewe kuzitumia,
Siri tukajitunzia, sio kila mtu kutujua,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Mapeni wamechukua, Mwingereza kuyatoa,
Mfukoni wakatia, lugha yetu kuiua,
Na uzungu kujitia, lipi wanalolijua?
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Hebu sasa angalia, Uchina imeshapaa,
Na India nayo pia, juu juu waelea,
Kisa yao kutumia, na si cha kung'ang'aniwa,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

Yarabi nakulilia, lugha kutuhifadhia,
Waovu kutowaachia, wasije wakakiua,
Kije sisi kutufaa, na vizazi vyetu pia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?

No comments: