Monday, August 26, 2013
FISADI AKISHAANZA
Nani amekwambia, eti kushiba ajua,
Huyo akishaanzia, daima huwa na njaa,
Tumbo huzidi panua, kama Jetwa hujakua,
Fisadi akishaanza, huwa haachi fasidi!
Fisadi mwana balaa, haramu hatokimbia,
Hutaka kuongezewa, hadi mapipa kujaa,
Raha akajionea, eti kwa k uangalia,
Fisadi akishaanza, huwa haachi fasidi!
Wa ndani humuibia, pasipo ya kutambua,
Cha nje kinapokuwa, kwa deni aweza ua,
Moja ataikimbilia, mia akaziachia,
Fisadi akishaanza, huwa haachi fasidi!
Nikahi anayoijua, ya nje ikitokea,
Kifua huikingia, wa ndani wakaasiwa,
Mitupu waliyokuwa, nani atajilambia?
Fisadi akishaanza, huwa haachi fasidi!
Fisadi mwana tamaa, na sifa huziogea,
Daima huzililia, jasmini yakatiwa,
Udi na uvumba pia, Uarabu kujitia,
Fisadi akishaanza, huwa haachi fasidi!
Hujaribu mwanakuwa, kuikusanya dunia,
Akashindwa kutambuwa, yeye ndiye atakiwa,
Kukusanywa na kutiwa, kwenye la sahau jaa,
Fisadi akishaanza, huwa haachi fasidi!
Mola atampangia, nini ataka fanyiwa,
Na siku kujiwekea, hakika akaitia,
Pasina kujitambua, nyuzi zilizobakia,
Fisadi akishaanza, huwa haachi fasidi!
Ya Afu nakuangukia, karama kunigawia,
La kesho wasilojua, miye nikalitambua,
Mbali nao nikakaa, na kuistadi dunia,
Fisadi akishaanza, huwa haachi fasidi!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment