Monday, September 23, 2013

AINA ZA UGAIDI



Mambo mengi ugaidi, jambo moja halijawa,
Nabonyeza kwako hodi,Upate kuyatambua,
Si moja kufaidi, na mengi kutokujua,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Ufisadi ugaidi, japo hatujalitambua,
Nao mkubwa mradi, duniani waenea,
Wengi wauona sudi, neema zinavyojaa,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Rabsha inajinadi, dhana kila kitu kuwa,
Kwalo sijaona idi, kufaidi sijajua,
Si mmoja ugaidi, asa umeshatambua,
Naupandisha mdadi, kuushusha natakiwa,

Wa maneno ugaidi, sasa unachipukia,
Wasema kwa ukaidi, na vitisho kuvitoa,
Hii haikuwa jadi, yatuzushia balaa,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Leo wanaofaidi, hawatakia kuachia,
Wafanza zote juhudi, wengi chini kudidimia,
Ili wabaki jadidi, juu wanashikilia,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Umeanza wa fisadi, mlo wote kupakua,
Hata dini kuritadi, lishe sababu ikiwa,
Akafanza ukaidi, kuipindua dunia,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Aidha wa ukaidi, na jeuri kuzitia,
Akachapwa mijeledi, mnyonge aliyekuwa,
Kisa ataka idadi, na vyanzo kuving'amua,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Kuna ule wa mdadi, na hasira kuvimbiwa,
Usimhofu Abadi, na vitisho kuvitoa,
Watu ukawafasidi, haki zao kuzitwaa,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Uongo pia mradi, nao ni ugaidi pia,
Kweli zisiwe ahadi, bali uongo kujaa,
Asojua hafaidi, hadi akitindikiwa,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Upo wa kutaradadi, utukufu kuombewa,
Au kwa zako juhudi, ukataka juu paa,
Asili ukakaidi, ikakutema dunia,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Kuna ule wa kijadi, na silaha kutumia,
Kwa bidii na juhudi, nguvu ukazitumia,
Cha wengi ukikinadi, na pengine kukitwaa,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Kuna ule wa magadi, pa chumvi ukaitia,
Na wa kutumia radi, watu ukawatumia,
Ajuaye ni Wadudi, vipi inavyotokea,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Upo ule wa hasidi, wengine kuwachukia,
Na ukiwapa ahadi, iwe isiyotimia,
Isikughasi fuadi, kawaida kwako kuwa,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Kuna ule wa baridi, mtu kimya kukaa,
Hana kadi, hana kodi, yake yanajiendea,
Amtanguliza Hadi, hata pasipotakiwa,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Na wasio maabuddi, Ibilisi huwavaa,
Yake waasiyakaidi, yeye akawatumia,
Haya yake ya mihadi, hadi mwisho kwenda kuwa,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Baraza nataradadi, tawakali tangulia,
Usiipate nakidi, na hasara kuingia,
Si mmoja ugaidi, sasa umeshang'amua,
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

Mwenye nguvu na mgodi, ndo' wa kumtambua?
Mwenye hisa na miradi, hatojanisingizia ?
Ayalilia Masudi, kuchora atarudia ?
Aina za ugaidi, hapa ninazianika!

No comments: