Monday, September 23, 2013

HIVI CHAMA KINA DIRA ?


KICHWA hutokijua, wala wapi ni mkia,
Kule unakodhania, uamuzi hutolewa,
Wao nao wangojea, wa chini kuja amua ?
Chama kinakosa dira, tukiokoe baharia!

Pembeni tuliokaa, dhaifu mabaharia,
Wakati umeshaingia, chama chetu kukitwaa,
Dira tukakipatia, baharini kuelea,
Chama kinakosa dira, tukiokoe baharia!

Mashaka tunayazua, kwa uongozi kufifia,
Wengi tuloachia, kazi yao kusifia,
Kombakomba walokuwa, eti vyeo wangojea,
Chama kinakosa dira, tukiokoe baharia!

Uoga umetujaa, chinichini twasemea,
Ukweli tunaujua, na batili nayo pia,
Vipi tunaendelea, kama vile hii kawa?
Chama kinakosa dira, tukiokoe baharia!

Mansuri kajitolea, ukweli kuutumbua,
Wazuka wa kuzomea, kumbe wanajishushua,
Ukweli ndio shujaa, daima tama adawa,
Chama kinakosa dira, tukiokoe baharia!

Watu tunawakimbia, wenyewe twajitumikia,
Pasi aibu na haya, kazi yetu imekuwa,
Huko tunakoeleka, walahi nakuhofia,
Chama kinakosa dira, tukiokoe baharia!

Kimya ninakikataa, tangazo hili kutoa,
Wenye chama watakiwa, ukweli kuutambua,
Tumeichagua njia, Mwalimu aliyokataa,
Chama kinakosa dira, tukiokoe baharia!

Kuongoza twatambua, ndilo tunalotakiwa,
Sasa tunaamriwa, kilingeni twatolewa,
Watu wanajionea, haya yote washangaa,
Chama kinakosa dira, tukiokoe baharia!

Tulishaongoza njia, si tu hapa Tanzania,
Afrika nako pia, pamwe nayo dunia,
Leo tumekuwa mkia, nyuma nyuma kufatia,
Chama kinakosa dira, tukiokoe baharia!

Falsafa imevia, wala hatunayo taa,
Gizani tunatembea, mambo kubahatishia,
Ya ndani wanaojua,  pakupiga wapajua,
Chama kinakosa dira, tukiokoe baharia!

Wafofaa twaachia, kazi zetu kuzikwea,
Ovyo wanajifanzia, kepesti na kukopia,
Majilisi kiingia, kichekesho kinakuwa,
Chama kinakosa dira, tukiokoe baharia!

Hawasomi wakajua,  na makosa kuyatoa,
Ndio wanaitikia, pasina kufikiria,
Uwakilishi wavia, na watu hili wajua,
Chama kinakosa dira, tukiokoe baharia!

Changamoto twaitoa, kwa upya kuzaliwa,
Wenye uchungu na nia,hivi sasa kujitoa,
Mkono nawaachia, sikufunga nafungua,
Chama kinakosa dira, tukiokoe baharia!


No comments: