Monday, September 23, 2013
Katiba ikija mbovu
Vijana waangalia, tunachowaamulia,
Mushkeli kikijaa, yasije yakawafaa,
Hatua watachukua, adhabu kali kutoa,
Katiba ikija mbovu, chama kuwa dhaifu!
Tuache jifikiria, kizazi kuangalia,
Ya leo tunayajua, kesho yasije zuia,
Maovu tuakayazua, kwenye pepo Tanzania,
Katiba ikija mbovu, chama kuwa dhaifu!
Viongozi wayajua, ndo kisa kuyakemea,
Isitumike hadaa, baharini twaelea,
Pepo zitatuumbua, kichangani kuelea,
Katiba ikija mbovu, chama kuwa dhaifu!
Macho tungeyafungua, tusome tuolosusia,
Mistari kujijua, kwa kujitafakaria,
Upofu tukijitia, wenyewe twaja kulia,
Katiba ikija mbovu, chama kuwa dhaifu!
Tusije kuvumilia, mbovu tukajapatiwa,
Mishipa tutaizua, na pumzi kulipua,
Nchi ikawa balaa, pasiwepo pa kukaa,
Katiba ikija mbovu, chama kuwa dhaifu!
Kwa hiari nayatoa, katikati nilokuwa,
Upande sijaegemea, mkweli wa Tanzania,
Haki nimepgiania, uhaini kuzuliwa,
Katiba ikija mbovu, chama kuwa dhaifu!
Maradhi nayatambua, kwa waliokisinzia,
Haya tukiyaachia, pabaya twaelekea,
Sangari kuing'ofoa, hiyo ni ya shamba dawa,
Katiba ikija mbovu, chama kuwa dhaifu!
Jalali twakulilia, uongozi kuzindua,
Wasije tuamulia, yawe ukimwi mpya,
Nchi itateketea, hali twaiangalia,
Katiba ikija mbovu, chama kuwa dhaifu!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment