Friday, September 6, 2013

D U N I A H A I W A P E N D I


Haiwapendi dunia, japo yawavumilia,

Uungu wanaojitia, na kiburi kuwajaa,

Huonekana mzaha, Mola wanamfanzia,

Haiwapendi dunia, uungu wajitiao!

 

Ovu wanaotishia, hata kwa waoto pia,

Watu wanawachukia, na kuwaona kinyaa,

Huwa mkubwa udhia, japo ukavumiliwa,

Haiwapendi dunia, waishio kwa vitisho!

 

Wafutuao vifua, na maguvu kutumia,

Ilhali wakiishiwa. upepo waja pungua,

Kinyamkera ni jaa, kila kitu huchukua,

Dunia haiwapendi, watunishao vifua !

 

Wajanja kupotezea, ni nadra kuridhiwa,

Kamba wanaachiiwa, za kwenda jitundikia,

Nao bila kujijua, vichwa wanavipanua,

Dunia haiwapendi, walokubuhu hadaa !

 

La mtu wasosikia, songombingo kujendea,

Hekima wakajitia, kwa busara kuitoa,

Rahisi kuvumiliwa, na sio kukubaliwa,

Dunia haiwapendi, ushauri wasotaka!

 

Wanaotaka kupaa, kwenye mwezi kutembea,

Hali ni hii dunia, wanayoikanyagia,

Huru watajisikia, ila deni walitwaa,

Dunia haiwapendi, wale wanaojiona !

 

Wale wanaounuia, kila mtu kuwajua,

Hata pasipowafaa, wakawa ni wa kuingia,

Nafsi hujichubua, dhihaka ikawajaa,

Dunia haiwapendi, wajifanzao sinema !

 

Wanaojilimbikizia, hadi wana kuvimbiwa,

Kisha wakajiachia, mitegoni kuingia,

Salama huwaachia, mbali nao ikakaa,

Dunia haiwapendi, waozao kwa fasidi !

 

Fahari wanaojitia, na mbwembwe kushangilia,

Dunia kuwazuzua, kisha ikawachezea,

Viumbe wasiojijua, si aghali kupotea,

Dunia haiwapendi, wale wanaojidai!

 

Ukuu wanaolilia, mafuu wengine kuwa,

Ngazi wakazitumia, kisha teke kuzitia,

Huku moyo wakomaa, uovu kuendelea,

Dunia haiwapendi, wale wanaojikweza !

 

Kelele waliojaa, hata kwa wasoyajua,

Katikati kwingilia, madebe wakapasua,

Huonekana nazaa, kicheko cha kuchefua,

Dunia haiwapendi, viumbe wenye kelele!

 

Ulimi wasiolea, ovyovyo kutumia,

Maneno wakayatoa, ya kuwakwaza raia,

Huonekana balaa, si wa kutegemewa,

Dunia haiwapendi, ulimi wasiochunga!

 

Uongo wanaoujua, wakashindwa ukataa,

Huwa ni waongo pia, wanafaa kuhofiwa,

Shimoni huja watia, machoni wawaangalia,

Dunia haiwapendi, waabuduo uongo!

 

Wageuzwao bidhaa, watu wakawanunua,

Kisha wakawatumia, kwa mengi yasiyokufaa,

Hawa ukiwaachia, hatiani unajitia,

Dunia haiwapendi, wageuzwao bidhaa !

 

Wasiokuwa na haya, maovu kutohofia,

Waziwazi wakavua, ilhali watembea,

Ni watu wa kuoghofya, ukiweza mbali kaa,

Dunia haiwapendi, haya wanaoikosa !

 

Kisasi waliojaa, na huruma kusinyaa,

Mola hatowaangalia, kiyama kikiingia,

Mgongo hugeuziwa, na motoni kwenda kaa,

Dunia haiwapendi, kisasi wanaojaa!

 

Mema hutarajia, uoza wakisifiwa,

Vichwa kukomalia, na mifuko kulegea,

Ila siku ikiingia, tundu hawatoshuhudia,

Dunia haiwapendi, wanaokosa huruma !

 

Watu wanaopakazia, makosa wakawazulia,

Kesi wakabambikiwa, na waovu kuwavaa,

Adhabu wakaipewa, chanzo wasichokijua,

Dunia haiwapendi,  wasingiziao watu !

 

NI wanaogeuziwa, na mamlaka zilokuwa,

Mola awaandalia, adhabu ya kurudia,

Motoni jivu wakawa, kisha tena kurejea,

Dunia haiwapendi, kibao wageuzao !

 

Rushwa wanaopalilia, na fanaka kupatia,

Miiba wapalilia, ya kesho wakifikia,

Nusura kutoijua, ila ni kuraruliwa,

Dunia haiwapendi, wazoea chauchau!

 

Shibe wasioijua, hadi tumbo kupasuwa,

Wala hadi kuvimbiwa, na magonjwa kuingia,

Adhabu ya wangojea, ilhali hai wakiwa,

Dunia haiwapendi, walao kama nguruwe!

 

Ya watu yaliyokuwa, kama majibwa wakawa,

Wakawa wenye ridhaa, pasina kweli kujua,

Wezi wakawatumia, ya kwao kujijengea,

Dunia haiwapendi, waishio kama mbwa

 

Dhuluma waliojaa, hata kwa wenye ukiwa,

Mola awaandalia, kibaya kilichokuwa,

Muhali kuwahurumia, wao wasipohurumia,

Dunia haiwapendi, wote wanaodhulumu!

 

Wanyonge wanaoonea, na vya kwao kuchukua,

Kubwa ardhi ikiwa, dunia inawajua,

Kuna siku watajua, ijapo kuwakataa,

Dunia haiwapendi,  watu wanaoonea !

 

Dharau wanaotia, kwa sana kujisheua,

Dunia huwabugia, kisha ikawacheua,

Mzoga ukaja liwa, na mafisi enye njaa,

Dunia haiwapendi, wanaofanza dharau !

 

Unafiki walojaa, huwakataa dunia,

Wanapoihitajia, 'no' huwatamkia,

Njiani wakaishia, na upwa kugaagaa,

Dunia haiwapendi, wale wenye unafiki !

 

Wanaozinyanyapaa, imani wasozijua,

Kumbe za kweli zikawa, hofu hawajaijua,

Laiti wakijitambua, watataka kufukiwa,

Dunia haiwapendi, watibuao imani!

 

Haki wanaonunua, wengine kuwauzuia,

Riziki kujipatia, wengine wakazuliwa,

Hadi ndani wakatiwa, uovu kwenda fanziwa,

Dunia haiwapendi, haki wanaonunua !

 

Haki wanaouziwa, matumbo huwaumbua,

Huja yakafutuliwa, kama baluni yakawa,

Ilhali wanakuwa, sinema kujionea,

Dunia haiwapendi, wanaouziwa haki !

 

Walokithiri tamaa, kila kitu walilia,

Hata vya  kuja waua, na uchizi kuwatia,

Si wa  kujitambua, viumbe wa kuhurumiwa,

Dunia haiwapendi, walokithiri tamaa !

 

Hudhani wanasifiwa, na mapambo kupambiwa,

Kumbe chini watumiwa, wenye njaa kuwafaa,

Siku wakijaishiwa, hupuputika manyoya,

Dunia haiwapendi, ila inawadanganya !

 

Kobe akadhindwa paa, duniani kureja,

Mgonjwa ajapokuwa, pasiwe wa kumwangalia,

Na hiyo ndiyo dunia, na mambo yake ni haya,

Dunia haiwapendi, wasomjua mgonjwa !

 

Fakiri wasoangalia,  haiwapendi dunia,

Mali wakijichumia, mchwa huja kujilia,

Na wana waliozaa, maskini hujifia,

Dunia haiwapendi, wasojua aso nacho !

 

Ukweli wanaofukia, na uongo kutumia,

Hawajui walaaniwa, ilihai wanakuwa,

Na siku huja ingia, vichwa vikawashangaa,

Dunia haiwapendi, wauzikao ukweli !

 

Wataniao dunia, huja mwisho kutaniwa,

Na hiyo  hiyo dunia, waliokiitania,

Na wa mwisho huambiwa, kicheko kikubwa huwa,

Dunia haiwapendi, wataniao dunia !

No comments: