Saturday, September 21, 2013

K A T I B A I J U U Y A W O T E



Juu atayejitia, asimame kutwambia,
Nani amemchagua, juu ya wengine kuwa,
Kigezo kilichotumiwa, na bei aliyotoa,
Katiba kitu kikubwa, wadogo sote raia !

Wapi imeruhusiwa, mstari kudadavua,
Nasi hatutambishia, njia tutamuachia,
Ila tunavyotambua, kwa juu hapatakuwa,
Katiba kitu kikubwa, wadogo sote raia !

Juu anayejitia, ataka kuichezea,
Usanii kujitia, asiyejua sanaa,
Ujuzi hakujaliwa, mabavu ayatumia,
Katiba kitu kikubwa, wadogo sote raia !

Usanifu kujitia, na uashi anajua,
Yule tunayetambua, hayo kamwe hakusomea,
Ni msiba twangojea, hali tunachekelea,
Katiba kitu kikubwa, wadogo sote raia !

Jengo akitujengea, laja kutuangukia,
Na wengine kufukiwa, kuzikwa hai wakiwa,
Wajifanzao wajua, kisha mbali wakakaa,
Katiba kitu kikubwa, wadogo sote raia !

Sisi wote ni raia, wakuu na wasiokuwa,
Hakuna alozidia, katiba yatuambia,
Vipi ikaja ikawa, mmoja juu akwaa?
Katiba kitu kikubwa, wadogo sote raia !

Ubinafsi twahofia, kwa madhara na nazaa,
Ndiio maana usia, huu wa historia,
Wote chini twarejea, nini tena kuambiwa?
Katiba kitu kikubwa, wadogo sote raia !

Chama kinapojitia, nchi kinaipindua,
Hila wakizitumia, ufidadi wajitia,
Batili kuitumia, halali wakaachia,
Katiba kitu kikubwa, wadogo sote raia !

Yao wajiandalia, na palizi kuitia,
Kwenye shamba la kuzua, kabaila kakodiwa,
Kondeni bomu zajaa, zisije tulipukia,
Katiba kitu kikubwa, wadogo sote raia !

Aihadaa Tanania, wakati haijasinzia,
Kono fukoni katia, halali avichomoa,
Vingine vyamwagikia, chini vikatapakaa,
Katiba kitu kikubwa, wadogo sote raia !

Yajichokea dunia, kuizoea mizaha,
Guu likijimbia, na kuutunga usahaa,
Siku itapowadia, uchungu tutasikia,
Katiba kitu kikubwa, wadogo sote raia !




No comments: