Angalia takataka, zazidi kuimarika,
Tunu hii ya hakika, kwake yeye Mwafrika,
Hajafa haujaumbika kabla hajawa taka,
Hawajali takataka, vipi wakujali wewe !
Ndivyo alivyoumbika, kihuru au mateka ?
Au analogeka, na juu waliioshika,
Akili zikakunjika, jipya kutokufanzika?
Hawajali takataka, vipi wakujali wewe !
Makwao wanapotoka, na kwa vimada kufika,
Kila kona kwapambika, kwa wingi wa takataka,
Haya yanakubalika, wala hawana mashaka,
Hawajali takataka, vipi wakujali wewe !
Kwa wageni kwarembeka, kwa Mwafrika ni mahoka,
Nchi ukiizunguka, hili sasa lajengeka,
Hata kulikosifika, sasa kunaharibika,
Hawajali takataka, vipi wakujali wewe !
Kila kttu wakishika, sasa chageuka taka,
Ila wao wapambika, na majoho kubebeka,
Huu nchi yanyongeka, vipi tutayaepuka?
Hawajali takataka, vipi wakujali wewe !
Akili za takataka, usafi hazitotaka,
Maana kunawirika, ni lazima kuchafuka,
Ndiyo wanayoyataka, hawawezi kugeuka,
Hawajali takataka, vipi wakujali wewe !
Ahadi ilishawekwa, muda unasubirika,
Siku yao kuja fika, wavune waliyotaka,
Na si mkosa Rabuka, mamboye ni ya hakika,
Hawajali takataka, vipi wakujali wewe !
No comments:
Post a Comment