Ndani ukijichimbia, ukaanza kuamua,
Kupe waliotulia, huzidi kujichimbia,
Hawana la kulijua, zaidi ya kuambiwa,
Udikteta ukiiva, watu hulishwa vibichi !
Amri huwa silaha, toka juu wakipewa,
Kugeuka si ridhaa, lazima kuitikia,
Hata likiwa ni baya, kwao zuri huambiwa,
Udikteta ukiiva, watu hulishwa vibichi !
Aidha roboti huwa, chama kimeshafyatua,
Si wa kufikiria, kujua wasilojua,
Gea ilishaingia, yote ndiyo kwitikia,
Udikteta ukiiva, watu hulishwa vibichi !
Hoja zote hufulia, na umma kunyanyapaa,
Wao wakajidhania, wajua wasiyojua,
Hadi machweo yakawa, shuka wanakimbilia,
Udikteta ukiiva, watu hulishwa vibichi !
Hutweta na kutetua, na vingama kupitia,
Ibura zikakimbia, na miujiza kupaa,
Majani mtu hutwaa, kama nguo akavaa,
Udikteta ukiiva, watu hulishwa vibichi !
Yaja tusiyoyajua, tena ya kutuumbua,
Wenzangu nawashtua, mmeacha kujitambua,
Na hakuna mkubwa udhia, kama mtu kutojijua,
Udikteta ukiiva, watu hulishwa vibichi !
Watu wanawahofia, huko mnakoelekea,
Njia mmeshapotea, kugeuka mwakataa ?
Na pori wanalijua, salama halijakuwa ?
Udikteta ukiiva, watu hulishwa vibichi !
No comments:
Post a Comment