Thursday, September 5, 2013

hivi kosa ni la nani?

Wakitamka bahali, hudhani Java natua,

Hushindwa tamka ghali, gari ukalisikia,

Hukambia kalili, kumbe kariri wambiwa,

Ni kosa la mwenye mali, au lake mhariri?

Hukutajia fahali, ng'ombe ukamdhania,

Kumbe umulimuli, na kung'ara kwa tabia,

Kiswahili dhofu hali,  wahariri waugua?

Ni kosa la mwenye mali, au lake mhariri?

Wakitamka ya hali, ulivyo huidhania,

Kumbe joto dalili, ndo wanalofikiria,

Wasemapo ya mahari, ndipo huchanganyikiwa,

Ni kosa la mwenye mali, au lake mhariri?

Mahali ndiyo mahari, hivi lini imekuwa,

Na kwanini mhariri, haya anayaridhia ?

Au hanayo habari, kwa yanayoripotiwa?

Ni kosa la mwenye mali, au lake mhariri?

Lini ikawa ni shali, hali ya kuwa ni shari,

Piri haijawa pili, hilo naona dosari,

Bado kwetu ni ajali, na ajari si sanjari,

Ni kosa la mwenye mali, au lake mhariri?

Kabuli huwa ukweli, haijawa ni kaburi,

Na ishara ni dalili, si hariri si dariri.

Na johari si johali, hilo kwa kweli athari,

Ni kosa la mwenye mali, au lake mhariri?

Kalili sio kariri, ni kidogo kitakuwa,

Wala reri sio reli, na wala haitakuwa,

Stairi si staili, mushkeli inakuwa,

Ni kosa la mwenye mali, au lake mhariri?

Ajira kama ajali, nasamehe wahariri,

Dampo la mwenye mali, huna ila ya hiari,

Ila wateja muhali, inataka ujibari,

Ni kosa la mwenye mali, au lake mhariri?

No comments: