Thursday, September 5, 2013

huwa kimya kimya


Mlipe vyema mlipa, siri atawafichia,

Chochote weza amua, haki yenu kujakuwa,

Na ataye wasumbua, haki yenu  huambiwa,

Kuna malipo kufuru, huwa kimya kimya!

 

Kuna kazi  za kupewa, na kanuni kujengewa,

Kama  unashateuliwa, sheria za kutetea,

Mifuko utajaziwa, na ziada kuchukua,

Kuna malipo kufuru, huwa kimya kimya!

 

Oisi hufunguliwa, na funguo kufungua,

Kila kitu wazi kuwa, waweza kujichukulia,

Nani wa kuangalia, cha mtu kisichokuwa?

Kuna malipo kufuru, huwa kimya kimya!

 

Sinema nazo sanaa, kuchota wabarikiwa,

Akili wakatwambia, wenzetu wanatumia,

Sisi tusiojaliwa, twabakia kufulia,

Kuna malipo kufuru, huwa kimya kimya!

 

Watunzi wazuzuliwa, waimbaji nao pia,

Bulungutu kugawiwa, kwa kazi zisizokaa,

Haziachi kufubaa, pesa weshazichukua,

Kuna malipo kufuru, huwa kimya kimya!

 

Wakala watuanzishia, wakawajaza jamaa,

Kufumba na kfuumbua, matajiri wanakuwa,

Kila ukiangalia, huoni tulilojaliwa,

Kuna malipo kufuru, huwa kimya kimya!

 

Ukuu wanagawiwa, na vilembe kufungiwa,

Majoho nayo kupewa, na senti zanye mkia,

Kila ukifuatilia, huoni unachoambua,

Kuna malipo kufuru, huwa kimya kimya!

 

Tume wanazizindua, mamilioni wakapewa,

Sasa nao watumbua, wafurahi Tanzania,

Kukumbukwa radhia, nini tena watalia?

Kuna malipo kufuru, huwa kimya kimya!

 

Ila ukiangalia, uwiano unavia,

Vijijini kwenye njaa, neema kutoijua,

Laana wamekamia, ubani kujichomea,

Kuna malipo kufuru, huwa kimya kimya!

 

Kiasi isipokuwa, amani huifagia,

Kiasi kikipotea, umoja hujibangua,

Kiasi isipokuwa, husuda huja kuua,

Kuna malipo kufuru, huwa kimya kimya!

No comments: