Hucheka nikisikia, yasiyokuwa najua,
Vivumishi kuvizua, utadhani wanapaa,
Ila ninavyoyajua, kutua yamekwishatua,
Fikra ndogo muhali, kuja kuzaa makubwa!
Hadithi imebakia, na nyingi zao tamaa,
Mioyo yanunuliwa, na akili nazo pia,
Hawana la kuamua, ila la kutarajiwa,
Fikra ndogo muhali, kuja kuzaa makubwa!
Nani amekuambia, finyu, pana litazaa,
Na chanya haitazaliwa, na hasi kinachokuwa,
Nyimbo wanajiimbia, kweli sintoitarajia,
Fikra ndogo muhali, kuja kuzaa makubwa!
Wanapenda kusikiwa, japo hewa wanatoa,
Aalli kisichokuwa, zaidi kukwepa njaa,
Wengine wanaugua, kukariri wasojua,
Fikra ndogo muhali, kuja kuzaa makubwa!
Wamezivaa kofia, matundu zilizojaa,
Zawavujia mvua, na hoja zisizokuwa,
Watu wanawashangaa, wao wanajisifia?
Fikra ndogo muhali, kuja kuzaa makubwa!
Hoja wainshauflia, na wengine waogea,
Kazi ni kurejearea, utadani mbovu pleya,
Wapenda kujisikia, hata kwa kisichonukia,
Fikra ndogo muhali, kuja kuzaa makubwa!
Juu waweza paua, na msingi hujatia,
Watu mnawakimbia, ushirikishi mwavua,
Kisha mnajisema, yakuwa na yasokuwa?
Fikra ndogo muhali, kuja kuzaa makubwa!
Chini mngejichimbia, na mizizi kuitia,
Ndipo mngeyafikia, ya matokeo kujua,
Kasi ipi ingekuwa, hilo noma twaawambia,
Fikra ndogo muhali, kuja kuzaa makubwa!
No comments:
Post a Comment