Monday, September 23, 2013
KATIBA YA WATANZANIA
Mola tunakulilia, batili kuikataa,
Halali kutupatia, kwa tunayoyatarajia,
Mama wa zetu sheria, mbele kumtangulia,
Katiba ya Tanzania, si ya chama kimoja !
Wamezuka waso haya, wajinga watudhania,
Ya kwao wapalilia, mchakato kupitia,
Ilhali tunajua, si halali yalokuwa,
Katiba ya Tanzania, si ya mtu mmoja !
Uchache wautumia, wingi wetu kufukia,
Sauti waikataa, yao wataka sikia,
Kisha waje kuamua, kizazi yasiyokifaa,
Katiba ya Tanzania, ya Watanzania wote !
Nchi yetu twaijua, na makundi yalokuwa,
Akili ukitumia, wawakilishi twajua,
Wiano kuangaliwa, kwa wenyewe kuchagua,
Katiba ya Tanzania, si ya chama kimoja !
Mfumo tulishaamua, wa wingi sio umoya,
Sasa yanayotokea, yarejesha historia,
Chama kinasimamia, kisichokistahilia,
Katiba ya Tanzania, si ya mtu mmoja !
Uwakilishi ni njia, watu wote kufikia,
Sio sisi kutugawa, kwa vijisenti kutoa,
Kisha wakateuliwa, ndiyo ndiyo kwitikia,
Katiba ya Tanzania, ya Watanzania wote !
Makundi tunayajua, na idadi nayo pia,
Hata waliokikataa, zamani kuhesabiwa,
Kipofu anawajua, barazani watakiwa,
Katiba ya Tanzania, ya Watanzania wote !
Wawapuuza raia, kama vile ni bidhaa,
Wengine wananunua, na mfukoni kutia,
Mwalimu angeshangaa, ukubwa wa kututia,
Katiba ya Tanzania, ya Watanzania wote !
Raia wanatambua, nani wamtarajia,
Barazani kwenda kaa, ili yao kutetewa,
Sasa wanachofanyiwa, zezeta waandaliwa,
Katiba ya Tanzania, si ya chama kimoja !
Wajuu waliokuwa, hawataki kusikia,
Maoni yanatolewa, dharau wanaitia,
Nchi utafikiria, haki yao imekuwa!
Katiba ya Tanzania, si ya mtu mmoja !
Kila wanaloambiwa, upuuzi wajionea,
Kama kawa kwendelea, pasi soni walla haya,
Ilhali tunajua, pabaya twaelekea,
Katiba ya Tanzania, ya Watanzania wote !
NCHI iliahidiwa, katiba bora kupewa,
Idumu miaka mia, kizazi kufurahia,
Leo tunashuhudia, ya mwaka mmoja wazua?
Katiba ya Tanzania, ya Watanzania wote !
NCHI iliahidiwa, katiba bora kupewa,
Idumu miaka mia, kizazi kufurahia,
Leo tunashuhudia, ya mwaka mmoja wazua?
Katiba ya Tanzania, ya Watanzania wote !
Rabi twakuhimidia, tuepushe na balaa,
Hekima kuwapatia, wakuu waliokuwa,
Zuri wakaliamua, kuokoa Tanzania,
Katiba ya Tanzania, ya Watanzania wote !
Rabana mwenye kujua, Bashiri uliyekuwa,
Upofu 'ngeliondoa, na busara kujalia,
Wakasimama raia, haki yao kupatiwa,
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment