Thursday, December 13, 2012

ASAKAYE KUSIFIWA


Kazi umejifanyia, na ujira unapewa,
Wajibu uliokuwa, wala haujatimia,
Ufanisi umevia, na ufanifu nazaa,
Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia !

Ziada hatujajua, kawaida inakuwa,
Kiasi inapingua, kwa wlaiotangulia,
Ila wakiri raia, mapambo  mwawazidia,
Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia !

Wastani wafatia, ajabu hajaibua,
Wachache waliopewa, na wengi hawajapewa,
Mizani ukitumia, pande gani yazidia?
Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia !

Saa hazijafikia, siku ya kuandikiwa,
Shinikizo unatia, ovataimu kupewa?
Mfanyakazi shangaa, weye wanakuumbua?
Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia !

Kama nguo ingekuwa, wengine wakazivaa,
Sura tu huondoa, zilezile zinakuwa,
Lakuajabikia, wallahi sijalijua,
Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia !

Mbio ingelkuwa, na wale mloanzia,
Wa mwisho mngelikuwa, zawadi mnalilia ?
Majaji watazubaa, washindwe kukuelewa,
Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia !

Riadha tunafulia, kumbe hivi inakuwa,
Tunataka zawadiwa, bila jasho kulitoa ?
Rahisi ilivyokuwa, kila mtu anuia,
Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia !

Rahisi ilivyokuwa, kutwaa bila kutoa,
Wengi wanakimbilia, nani atawasumbua,
Kazi tusingechachua, wengi wangelikimbia,
Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia !

Katiba inatakiwa, viwango kutuwekea,
Kati isipofikia, kofia ni kuwavua,
Kelele kutotupigia, stahili isokuwa,
Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia !

Kandanda twaondolewa, kisa hiki kimekuwa,
Hatujipangi muruwa, na ratiba twakataa,
Uwekezaji wavia, na motisha zafifia,
Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia !

Mazingira mwatakiwa, yote kuyaangalia,
Vipimo mkachukua, vigezo kujiwekea,
Haya mnapojitia, aibu mwajiombea,
Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia !

Kilio mkiangua, uongo tutakijua,
Msiba wa kujitakia, jirni hukukimbia,
Nduguzo wakaachiwa, wenyewe kukufukia,
Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia !

No comments: