Thursday, December 13, 2012

HAO NDIO HAO HAO

HUJIFANZA Sio wao, lakini ni hao hao,
Kazi ni kupiga mwao,  na ukora wa vilio,
Kelele mtindo wao, kuepa ni kazi yao,
Ya jibwa mbweka wowowo, hao ndio hao hao!

Hufatwa paka miyao, kila akilia taoo,
Wakenda nazo chepuo, vita visivyo na ngao,
Mazoezi mazomeo, na dharau za ng'oo,
Ya jibwa mbweka wowowo, hao ndio hao hao!

Hao si kitu washikao, kuachia kazi yao,
Halisimami jambo lao, ila kwa nguzo za teo,
Yakishafika machweo, ndio macho wafungao,
Ya jibwa mbweka wowowo, hao ndio hao hao!
Haviishi vipepeo, kufukuza harufuyo,
Vigelegele vimeo, ndivyo wavitumiao,
Ni washindwa washindao, na madhambi wavunao,
Ya jibwa mbweka wowowo, hao ndio hao hao!

Ni milango wafungao, yao si tusikiayo,
Akili nje waachao, utupu ndani uwao,
Ni ni walewayo, isipokuwa uchoyo,
Ya jibwa mbweka wowowo, hao ndio hao hao!

Si watu wajengao, huwa ni wabomoao,
Sio paa wawekao, ila ndio waezuwao,
Maji yao kwenye ndoo, umaskini ngao yao,
Ya jibwa mbweka wowowo, hao ndio hao hao!

Na hili ni jaribio, pango nyoka wamtoao,
Kisicho na muelekeo, hakina matamanio,
Wasiotumia kioo, sura si waijuayo,
Ya jibwa mbweka wowowo, hao ndio hao hao!

No comments: