Thursday, December 13, 2012

U R I T H I


BABA anamhofia, ataiaga dunia,
Naye anajiandaa, urithi kuuchukua,
Fursa azichambua, pahali pema kukaa,
Ukubwa aulilia, kurithi mali za chama ?

Kisa nimehadithiwa, mizungu kilichotiwa,
Ngano ya kuenguliwa, toka tambo za dunia,
Inayotia fadhaa, na  hamasa kupungua,
Ukubwa aulilia, kurithi mali za chama ?

Kumbe nilivyoyajua, sivyo yalivyotokea,
Kielelezo si dawa, zaidi walichengua,
Ndani wakayafikia, mimi nisiyoyajua,
Ukubwa aulilia, kurithi mali za chama ?

Fadhaa yawaumbua, neno hili kusikia,
Uraibu umekuwa, pombe waisiyoelewa,
Mlevi sasa kichaa, kila mtu abambua,
Ukubwa aulilia, kurithi mali za chama ?

Kumbe laini kikiwa, ugumu ndani hulea,
KIla kinachong'aa, hakiachi kufubaa,
Navyo vinavyovutia, mvuto huja kwiishiwa,
Ukubwa aulilia, kurithi mali za chama ?

Rai niliitengua, haikuwa ya raia,
Mwenzi aliyezidiwa, wala hakuwa mzawa,
Mwana aliyejitia, hakuwa Mtanzania?
Si mshairi wa chama, na wala haitakuwa !
Ukubwa aulilia, kurithi mali za chama ?

Watumwa waliokuwa, danguroni wamekaa,
Nta sasa wazaa, na mnato kuutia,
Mzinga kupalilia, kuvuna ya ushujaa?
Ukubwa aulilia, kurithi mali za chama ?

Hatua wasiotwaa, aibu wanatutia,
Umma wahofu ubia, walikwishauandaa,
Wafanzao wayahua, na kwetu sisi hadaa,
Ukubwa aulilia, kurithi mali za chama ?


No comments: