ZA dini zilizokuwa, na ukabila kutia,
Kwao kupalilia, magugu kwetu kwotea,
Tunashindwa kwelewa, nini chapaliliwa ?
Ni nini lapaliliwa, harambee za mnafiki!
Siri hatujaijua, sinema twajionea,
Wahariri wakatia, kurasa isotakiwa,
Na tivii kutumia, na haja pasipokuwa,
Ni nini lapaliliwa, harambee za mnafiki!
Papi pasipougua, kwetu hapa Tanzania,
Kumoja kukatibiwa, na kwingine kuchiwa,
Kadari kama ikiwa, hilo basi naridhia,
Ni nini lapaliliwa, harambee za mnafiki!
Ila ninayoyajua, cheo si kupendelea,
Kwenu ukawajengea, wengine wakafulia,
Neema ukaigawa, jinsi unavyojisikia,
Ni nini lapaliliwa, harambee za mnafiki!
Imani ukazigawa, hawa ukasaidia,
Wengine ukawaambaa, na ya kwao kupuuzia,
Mioyo hufa hisia, na upendo kupotea,
Ni nini lapaliliwa, harambee za mnafiki!
Mbegu mlizochukua, ardhi yazikataa,
Mkilazamisha wakiwa, wanawenu kuja kuwa,
Hili msipolijua, mtakuja kushangaa,
Ni nini lapaliliwa, harambee za mnafiki!
Hadithi zasimuliwa, wanafiki kuwajua,
Ahadi zao nazaa, kweli haitatokea,
Naye akiaminiwa, usadiki hatojua,
Ni nini lapaliliwa, harambee za mnafiki!
Na mijini wamejaa, sasa wayaogelea,
Kawaida kufulia, pasi wakaingojea,
Bila ya maji kutia, na moto umekolea,
Ni nini lapaliliwa, harambee za mnafiki!
Kijijini natulia, moyo wangu kuufua,
Kwaniridhi, naridhia, nakuona maridhia,
Hakika hii ni njia, pepo katika dunia,
Ni nini lapaliliwa, harambee za mnafiki!
No comments:
Post a Comment