Siku nikiziringia, na miezi kufatia,
Miaka nikanuia, duniani nitakaa,
Dakika sikuchukua, ng'ambo nimesharushiwa,
Laiti ningelijua, kuishi kumbe masaa !
Laiti ningelijua, nisingetia udhia,
Roho safi ningekuwa, kila mtu kumwangalia,
Wema ningeunuia, watu wote kugawia,
Laiti ningelijua, kuishi kumbe masaa !
Huruma ningeilea, mayatima kuwalea,
Kama wana wangekuwa, kwa mapenzi kuyanoa,
Ukiwa wasingejua, kama wangu wangekuwa,
Laiti ningelijua, kuishi kumbe masaa !
Fakiri wasingekuwa, wale ninaowajua,
Zaka ngeliwagawia, umaskini kuutoa,
Kisha kuwasaidia, hadi yao yakakua,
Laiti ningelijua, kuishi kumbe masaa !
Ya dini ningeyajua, yake nikapalilia,
Tajiwidi kunuia, mengine nikahofia,
Imani ingenijaa, sio mambo ya ruia,
Laiti ningelijua, kuishi kumbe masaa !
Ujana ningetumia, kwa wengine kuwafaa,
Dini ningejisomea, kihiyo nisingekuwa,
Kiarabu ningejua, na hija nisingeachia,
Laiti ningelijua, kuishi kumbe masaa !
Umri ningeutumia, ibada kujifanzia,
Anasa ningekimbia, pamwe kujitangazia,
Yangu ningeangalia, sabilllahi yakawa,
Laiti ningelijua, kuishi kumbe masaa !
Mali nisingeichezea, kwa fujo kuitumia,
Anisi kusainia, na ukafiri kufaa,
Haki ningepigania, wanyonge kusaidia,
Laiti ningelijua, kuishi kumbe masaa !
Elimu ningeitumia, kwa wengine kugawia,
Mwisho nisingefikia, milango mingi kwingia,
Hadi China kuingia, yao nikajisomea,
Laiti ningelijua, kuishi kumbe masaa !
Afya isingenifaa, pasina wengi kufaa,
Yao nikaangalia, hadi siha wakajawa,
Hapo ningeliridhia, laiti ningelijua,
Laiti ningelijua, kuishi kumbe masaa !
No comments:
Post a Comment