PAPO kwa papo kuamua, pasi kuwa na bajeti,
Sifa za kuserubukia, shukrani kuambua,
Watu wakasujudia, na viatu kurambia,
Nchi yanaiyumbisha, maamuzi ZIMAMOTO !
Hayo ya kujinyanyua, walipokwishagukia,
Wakaondoa udhia, matope kwenda ondoa,
Huruma wakajiuzia, kwenye njaa na ukiwa,
Nchi yanaiyumbisha, maamuzi ZIMAMOTO !
Mamlaka kuyazoa, mtu ukajilimbikia,
Ukabaki kuamua, na wengine kushangaa,
Haiwi kushangilia, ubaya ukitiokea,
Nchi yanaiyumbisha, maamuzi ZIMAMOTO !
Nchi inayo mikoa, kama nchi ilokuwa,
Uhuru isipopewa, nchi tutaichezea,
Mbali hatuafikia, tutaanza kupagawa,
Nchi yanaiyumbisha, maamuzi ZIMAMOTO !
Inatakiwa mikoa, mipango yao kuzua,
Na uongozi ridhaa, wenyewe kujichagua,
Hatua wakajipangia, wapi wataka fikia,
Nchi yanaiyumbisha, maamuzi ZIMAMOTO !
Dar wakingojea, yao kuja kuamua,
Mikoa itafubaa, na riadha kufulia,
Mbali hawatafikia, kuchekwa iwe tabia,
Nchi yanaiyumbisha, maamuzi ZIMAMOTO !
Uchumi kuunyanyua, wakazi wanatakiwa,
Yao wakayamua, na ulua kuutia,
Kadiri wakaagua, wawezavo jinasua,
Nchi yanaiyumbisha, maamuzi ZIMAMOTO !
Nasaha nimeitoa, naomba hoja kutoa,
Manani akajalia, upevu kuufikia,
Nchi ni kubwa gunia, sio rahisi kujaa,
Nchi yanaiyumbisha, maamuzi ZIMAMOTO !
No comments:
Post a Comment