Thursday, December 13, 2012

Makombora yanarudi

 YATUPWA kuhilikia, safu wakazipangua,
Asubhi kiingia, mipango wanajipangia,
Jioni ikiishia, tathmini hutolewa,
Makombora yanarudi, kule yalikotokea !

Hadithi kuendelea, hurushwa yakarejea,
Mwamvuli wahofia, mlengwa anatumia,
Uyahudi wangejua, huyo wangemnunua,
Makombora yanarudi, kule yalikotokea !

Wabaki kusingizia, adui kawarushia,
Kumbe ilivyokuwa, yenyewe yajirudia,
Siri hawajaijua, wanazidi kuumia,
Makombora yanarudi, kule yalikotokea !

Aliko hawajajua, nasibu waitumia,
Kapelekewa hidaya, wala hazikupokelewa,
Wadhani ana  kinaya, hayajali ya dunia,
Makombora yanarudi, kule yalikotokea !

Ganzi limeshaingia, ovoovyo yarushiwa,
Lengo sijalitambua, wala pia yake nia,
Hadhira inashangaa, kitali kinavyokuwa,
Makombora yanarudi, kule yalikotokea !

Na mimi najiachia, mlinzi atanifaa,
Kadari sijaijua, pengine hii ndo njia,
Wito nilishaitikia, hutoweza kunitoa,
Makombora yanarudi, kule yalikotokea !

Hili sikuigilizia, starehe naijua,
Tena ninafurahia, kulikosa si ridhaa,
Wanyonge ni yangu bia, hunywa hadi nikalewa,
Makombora yanarudi, kule yalikotokea !

Hayanipiti masaa, bila kuwaulizia,
Hali zao kuzijua, na nini wapungukiwa,
Sinacho nitakitoa, kukopa nilichopwa,
Makombora yanarudi, kule yalikotokea !

Mkononi huachia, mtupu nikabakia,
Hali nikiangalia, h aziwezi fanania,
Ila raha naijua, wala siwezi kulia,
Makombora yanarudi, kule yalikotokea !

Nderemo inapokuwa, peponi hujisikia,
Na kilio wakilia, ninauvaa ukiwa,
Yao niemshakusudia, ya kwangu budi yakawa,
Makombora yanarudi, kule yalikotokea !

Laiti mngelijua, kusita isingekuwa,
katika hii dunia, uongozi ni kufaa,
Uongozi wa kubwia, na starehe karaha,
Makombora yanarudi, kule yalikotokea !

Hesabu nishahisabia, wa sikio, kusikia,
Ulimi sikuachia, ila kwa kujizuia,
Lengo nalitarajia, Mwenyezi atajalia,
Makombora yanarudi, kule yalikotokea !

No comments: