Thursday, December 13, 2012

Kwenu ukiwajengea

 Kwenu ukiangalia, na kwingine saidia,
Haki kuianglaia, usawa ukatimia,
Sio huku kuchukua, kule tu ukawafa,
Kwenu ukiwajengea, na kwingine angalia!

Mizani kusimamia, usawa kuangalia,
Haki ukashadidia, bila kitu kupungua,
Rehema mkatunukiwa, kwa dhuluma kuiondoa,
Kwenu ukiwajengea, na kwingine angalia!

Katiba ninavyojua, ulinganifu sheria,
Pasiwe wa kuonewa, wala wa kupendelewa,
Sasa kinachotokea, mashaka kinatutia,
Kwenu ukiwajengea, na kwingine angalia!

Kwa wapinzani huvia, tawala wakachanua,
Au swahiba pakiwa, mambo yatazinduliwa,
Kwa wengine kunapwaya, nani wa kuangalia ?
Kwenu ukiwajengea, na kwingine angalia!

Kwa wakubwa nasikia, ridhaa wakajengewa,
Wengine wakililia, hiyo ndoto waambiwa,
Mizani naihofia, pande inaegemea,
Kwenu ukiwajengea, na kwingine angalia!

Wanakokupachagua, kwa wakubwa walokuwa,
Wadogo yarukwa njia, hadi mbali kuendea,
Mkubwa palipokuwa, sasa ndio huangaliwa,
Kwenu ukiwajengea, na kwingine angalia!

Hili sijaliridhia, wala sintolliridhia,
Hofu yangu nawambia, ila ninaidhania,
Jema halitajaliwa, mabaya laja kuzua,
Kwenu ukiwajengea, na kwingine angalia!


No comments: