Thursday, December 13, 2012

Hii kwako kumbukumbu

 Unadhani umefika, na garini umeshuka,
Hakika umepotoka, mwishowe haujafika,
Safari ina masika, ni vuli ulikotoka,
Hii kwako kumbukumbu, safariyo haijesha!

Hii siyo ya haraka, kwa umbali yasifika,
Mwanzo wake wa marika, miaka kuhesabika,
Mwisho wake  si shaka, tamati inatoweka,
Hii kwako kumbukumbu, safariyo haijesha!

Na wanaoweweseka, hudhania wamefika,
Mikoba wakaishika, huku wataka kushuka,
Ila wakijazinduka, popote hawajafika,
Hii kwako kumbukumbu, safariyo haijesha!

Tao ukierevuka, hili halina mashaka,
Mtawa keshayandika, mtandaoni kaweka,
Ukitaka elimika, tembelea kupevuka,
Hii kwako kumbukumbu, safariyo haijesha!

No comments: