Wageni wakiingia, sithaminiwi wajua,
Wao kinachafia, aitivii inakuwa,
Dharau siichukii, mzawa sinayo hadhi!
Hadhi sijathaminiwa, na hali waichimbua,
Heri wamejigawia, makiwa kunigawia,
Hawapo kuninyanyua, ila kunishindilia,
Dharau siichukii, mzawa sinayo hadhi!
Yao wanafatilia, kwa karibu kwangalia,
Doti wanaitambua, hadi nukta kulea,
Hawawezi kuachia, cha kwao kikapotea,
Dharau siichukii, mzawa sinayo hadhi!
Vya wengine hubeua, udhalili kuvitia,
Kisha wakavitifua, kama wasipotumia,
Yatima kumuibia, kisha utumwa kumtia,
Dharau siichukii, mzawa sinayo hadhi!
Jadi yangu kufulia, wengine kusaidia,
Ni jiwe kukanyagia, ng'ambo kwenda kuvukia,
Heshimake naijua, kingine sintolilia,
Dharau siichukii, mzawa sinayo hadhi!
Sawa wote tungekuwa, isingekalika dunia,
Kipawa ukijaliwa, si wote watapewa,
Wewe unayoyajua, vipi wao kuyajua,
Dharau siichukii, mzawa sinayo hadhi!
Leo hii waijua, ghaibu wameshafulia,
Hapa ndipo hudhania, huwa mwanzo kuishia,
Wewe unalielewa, maisha yaendelea,
Dharau siichukii, mzawa sinayo hadhi!
Ni hatua kupitia, mwisho hatujafikia,
Wengi inawazudua, wakadhani wametua,
Kisha wakajifanyia, ya dhuluma na izaya,
Dharau siichukii, mzawa sinayo hadhi!
Yarabi nakusifia, mjua mwenye kujua,
Macho umenifungua, kuiona yangu njia,
Zaidi sintolilia, ila kuniangalia,
Dharau siichukii, mzawa sinayo hadhi!
No comments:
Post a Comment