Tivii wazinunua, ya kwao kutangaziwa,
Hata ushuzi ukiwa, mradi una rupia,
Kung'ara kwenye tivii, siri ya mafanikio?
Bishara zinatukia, hadhi sasa zinapewa,
Ukubwa kutangaziwa, pasina ya kusinzia,
Kama hukutangaziwa, kujitangaza amua,
Kung'ara kwenye jarida, siri ya mafanikio?
Kwenye habari kivia, na lako huwa lavia,
Wapaswa twaa hatua, usikose angaziwa,
Hata kama kulipia, utaja kurejeshewa,
Kung'ara kwenye tovuti, siri ya mafanikio?
Cheo ukikichukua, gharama ndogo ikawa,
Kwingi utakukwambua, hata mawe nayo pia,
Hubinywa damu kutoa, kwa dawa ukatumia,
Kung'ara kwenye tivii, siri ya mafanikio?
Shani imetufikia, ya mazuri kutononoa,
Na sauti kusikiwa, hata na wenye mafua,
Vigugumizi wakawa, kwenye vyombo ni fasaha,
Kung'ara kwenye jarida, siri ya mafanikio?
Uchumi wa zawadiwa, bila ya kutumikia,
Enzie zimefikia, wajuao watambua,
Jasho wanaolitoa, papo hapo hubakia,
Kung'ara kwenye tovuti, siri ya mafanikio?
Kizungumkuti kikawa, dhihaka kupaliliwa,
Nami hilo nimeng'amua, ang'arae atumiwa,
Mishipi washilkilia, mwanasesere akawa,
Kung'ara kwenye tivii, siri ya mafanikio?
Itihari hatakuwa, kaziye kutumikia,
Hufanza la kuambiwa, hutumwa kutumikia,
Nchi atawauzia, bila ya kuulizia,
Kung'ara kwenye jarida, siri ya mafanikio?
Ni nani asiyejua, hadhihi ya kuambiwa,
Huyo wa kukimbilia, kitu gani afatia,
Nini aenda fichua, au ulinzi kutoa ?
Kung'ara kwenye tovuti, siri ya mafanikio?
No comments:
Post a Comment