Thursday, December 13, 2012

Lenu langu litakuwa

Wanyonge wanapokuwa, na mimi nitaingia,
Lao nikalichukua, mpka langu likawa,
Ndicho nilichoumbiwa, musrati kufwatia,
Ya kwangu kufanikiwa, lenu langu kujakuwa!

Sikuumbiwa dunia, njii hii napitia,
Lengo nimejiwekea, uangavu kufikia,
Kuona msiyojua, wala kuyafikiria,
Ya kwangu kufanikiwa, lenu langu kujakuwa!

Hili si la kuombewa, ni tunu ikijaliwa,
Mimi nalifurahia, kuishi naaazimia,
Msongo kwangu likawa, shinikizo kunitia,
Ya kwangu kufanikiwa, lenu langu kujakuwa!

Maisha nakadiria, taishi kutumikia,
Vingine naviachia, hili kwake nahamaia,
Nikaanzisha ubia, milele kuendela,
Ya kwangu kufanikiwa, lenu langu kujakuwa!

Inshallah naitia, siachi kukumbukia,
Neema najiombea, na kinga nikapatiwa,
Akitacho Jalia, na hakika ndilo huwa,
Ya kwangu kufanikiwa, lenu langu kujakuwa!

Hili ninalielewa, vingine sijafikiria,
Nafuai nimeitoa, ruksa sijajaliwa,
Yeye ndiye huamua, mimi wa kufatilia,
Ya kwangu kufanikiwa, lenu langu kujakuwa!

Nia akibarikia, lake ndilo hutimia,
Mimi atanitumia, abdi niliyekuwa,
Lake nikaitikia, na kazi kumfanzia,
Ya kwangu kufanikiwa, lenu langu kujakuwa!

Muhula akinigea, vyema kutumikia,
Hadi nitapofikia, wengine wakachukua,
Yake akaniridhia, na mimi kumridhia,
Ya kwangu kufanikiwa, lenu langu kujakuwa!

Akhiri amesikia, yangu atayaridhia,
Nakili lililokuwa, uwakili sijapewa,
Ila kushuhudia, kwa lile ninalojua,
Ya kwangu kufanikiwa, lenu langu kujakuwa!

No comments: