Thursday, December 13, 2012

LIPI NILILOFANZA

Ukubwa wa kujipuliza, kama mwana na kondomu,
Huu ninaupuuza, hauwezi kwangu dumu,
Ni ajizi ya ajuza, mabinti kuwa hirimu,
Lipi nililolifanza, hata niitwe mkubwa!

Ni muhali sintoweza, moyo hautojihimu,
Ningekuwa Mwanaweza, ningekuwa binadamu?
Bei sijajiagiza, nisije kushushuliwa,
Lipi nililolifanza, hata niitwe mkubwa!

Wala yangu si ya pweza, mikono kujikirimu,
Naiona miujiza, na mie siifahamu,
Nafanza ninachoweza, mengine yake Karimu,
Lipi nililolifanza, hata niitwe mkubwa!

Watu sitaki kuteza, na kisha kuwadhulumu,
Mwili wangu nautuza, uhai na marehemu,
Nikawaponza mafunza,  yangu wasiwe na hamu,
Lipi nililolifanza, hata niitwe mkubwa!

Ninakuomba Muweza, unyonge unikitimu,
Nizuie kujikweza, mahala nisipodumu,
Ngazi yangu kuongeza, mbele ya umarehemu,
Lipi nililolifanza, hata niitwe mkubwa!


No comments: