YUMKINI siioni, ya kunitukuza shani,
Matamanio nahini, naijua tathmini,
Utawa sijabaini, na uwalii sidhani,
Sijaiona thamni, niringie kitu gani!
Naitafuta thamani, kutoka kwa aliinsani,
Waniweke kundi gani, ubinadamu kuwini,
Kisha kwa hatua gani, uishapo uzaini,
Sijaiona thamni, niringie kitu gani!
Naitafuta imani, pasina ya usononi,
Aidha pia amani, pasina huu utani,
Na umoja kuauni. kwa wakweli wumini,
Sijaiona thamni, niringie kitu gani!
I chini yangu mizani, najiona bado duni,
Dhalili ni mashakani, na dhaifu akilini,
Ubora sijabaini, ningalipo kichakani,
Sijaiona thamni, niringie kitu gani!
Haki sijaithamini, nikaitia moyoni,
Nguli wananirubuni, kuwaatia zaini,
Nawahofia Kaini, waliopo duniani,
Sijaiona thamni, niringie kitu gani!
Kwa ukweli mhaini, na siasa wadhamni,
Nikiitia moyoni, waitoa akilini,
Nabebeshwa mkononi, kisicho nayo thamani,
Sijaiona thamni, niringie kitu gani!
Wako wapi wenye shani, yangu wakayadhamini,
Nikimbie nukstani, na kujihini moyoni,
Nikaipata amani, akilini na rohoni?
Sijaiona thamni, niringie kitu gani!
Rabana wewe rubani, tena wa juu angani,
Anga zako hawaoni, wanaishia pembezoni,
Niwe wako aliamini, unisafishe moyoni,
Sijaiona thamni, niringie kitu gani!
No comments:
Post a Comment