Thursday, December 13, 2012

MSHAIRI WA WANANCHI

 KUSIFU yao napwaya, vipi watanisikiya,
Hao wameshazoea, sikuzote kusifiwa,
Washairi  huwalea, uongo wakapepea,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Elimu ikapwelea, kama watoto wakawa,
Hukariri pasi jua, kauli wanazotoa,
Wakafulia sanaa, kwa kuvalishwa manyoya,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Wengi watanunuliwa, kwenda kuwatumikia,
Tenzi wakawaimbia, uongo zashehenea,
Vipimo wakatumia, usawa visivyotiwa,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Wajibu huusifia, haki inayotakiwa,
Mtu akijifanyia, na ujira akapewa,
Ni uzushi kuingia, kwalo hilo kumsifia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Mahitaji twayajua, ya msingi yaliyokuwa,
Vipi utamsifia, jukumu kuangalia?
Stahili naijua, sifa si haki kupewa,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Barabara zatakiwa, sisi sote kutumia,
Vipi tutakusifia, eti kwa kutletea?
Madaraja nayo pia, budi yakawepo pia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Madaraja nayo pia, budi yakawepo pia,
Ni kazi  kuangaliwa, hao waliopangiwa,
Marufuku kusifiwa, ikiwa hivyo nazaa,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Maji kote yatakiwa, watu wanayalilia,
Vipi wataka sifiwa, wajibu ukitimia,
Ajabu ingelikuwa, ya kwako kunyunyizia,
Madaraja nayo pia, budi yakawepo pia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Umeme unapwelea, gharama watubambikia,
Kiwizi watuibia, tayari watupunguzia,
Uniti chache zikawa, wiki kutosaidia,
Madaraja nayo pia, budi yakawepo pia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Kisha watuzungukia, zaidi kutuongzezea,
Nadhani wanatania, wafanyalo wajua,
Wameishatuzungukia, ujanja watufanzia,
Madaraja nayo pia, budi yakawepo pia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Tisini asilimia, sio waliopaiwa,
Sasa wataka kamua, kumi tuliojaliwa,
Hata mawe yanalia, uhuni kutufanyia,
Madaraja nayo pia, budi yakawepo pia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Shrika kujichungua, hivi laona udhia,
Naona mijitu yajaa, na kazi isiyokuwa,
Nchi wanaichezea, tabu tupu inakuwa,
Madaraja nayo pia, budi yakawepo pia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Hili mkilinchungua, mianya tele yajaa,
Nyufa zinazotanua, gharama kutuzidishia,
Na wakubwa wanajua, ubazazi kuamua,
Madaraja nayo pia, budi yakawepo pia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Vijiji vyasahauliwa, mijini tumehamia,
Hata waliozaliwa, sasa wanakuchukia,
Hii siachi shangaa, wapi tunaeleeka,
Madaraja nayo pia, budi yakawepo pia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Fikra tumefulia, ukubwa kuugombea,
Wajinga tulivyokuwa, haya tunayaridhia,
Laiti tungelijua, ukubwa kutumikia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Laiti tungelijua, ukubwa kutumikia,
Watu wapate kukua, kiuchumi kwendelea,
Na kijamii wakawa, ustawi waujua,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Wanaojisaidia, wenyewe kuendelea,
Vionozi  hawajawa, mamluki wa kujifaa,
Yao yakishatimia, yenu hawatoangalia,
Laiti tungelijua, ukubwa kutumikia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Wengi wanaolilia, ukubwa hili huzua,
Wataka yao kupaa, sio yenu kutatua,
Kura mkiwaachia, mwaja kesho kujutia,
Laiti tungelijua, ukubwa kutumikia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Thamani wamepania, ya kwenu kupungua,
Sio kitu mlokuwa, kura mkishazitoa,
Huuzwa na kununuliwa, jinsi wanavyoamua,
Laiti tungelijua, ukubwa kutumikia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Na mimi nawazindua, ili mpate kujua,
Vipi watafurahia, wapate kunitambua,
Watataka nifukia, pasiwe wa kunisikia,
Laiti tungelijua, ukubwa kutumikia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Kifo watashangilia, na rambirambi  kutoa,
Mwehu niliyekuwa, ya wajinga kutetea,
Tena nilipungukiwa, na zaidi kukashifiwa,
Laiti tungelijua, ukubwa kutumikia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Mola ninamuachia, malengo kusaidia,
Ukiwani kuwatoa, niwezao kuwatoa,
Kuchoka nitakataa,  hadi siku ya kiyama,
Laiti tungelijua, ukubwa kutumikia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Ukweli wanaoua, rafiki hawatakuwa,
Ubaya kunizulia, na mengi kusingiziwa,
Imeoza Tanzania, kwa uongo kuulea,
Laiti tungelijua, ukubwa kutumikia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Wasafi mkichagua, watakuja ligundua,
Yangu watashangilia, na ukweli kuujua,
Siku hiyo kujakuwa, nisiwe wenda ikawa,
Laiti tungelijua, ukubwa kutumikia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

Ila nitalisikia, kaburini kuambiwa,
Moyo nikaufungua, kama ua kuchanua,
Niridhie Tanzania, nayo ikaniridhia,
Laiti tungelijua, ukubwa kutumikia,
Mshairi wa wananchi, wakubwa watanipenda ?

No comments: