Thursday, December 13, 2012

KWA NYOTE MLIONIPENDA


Shukurani nazitoa, kwa wote walionipenda,
 Hisani walonigea, na maisha kunifunda,
Ingawa wamenipotea, kwangu bado ni mawanda,
Wote walionipenda, shukurani nazitoa !

Kuishi tuliokaa, tukawa pete na chanda,
Asante nawatumia,  na ningali nawapenda,
Siachi wafikiria, na dua zenu naganda,
Wote walionipenda, shukurani nazitoa !

Haziniishi ruia, kichwani zinavyotanda,
Sura ninajionea,  kama pichani zaganda,
Na sauti husikia, za vicheko vikitanda,
Wote walionipenda, shukurani nazitoa !

Maisha yalikataa, pamoja sote kuwanda,
Nasibu hatukupewa,  kwa karibu tukaranda,
Yote tumeyaachia, yalazimu kusarenda,
Wote walionipenda, shukurani nazitoa !

Umbali watuzuia, kwa miaka nazo nyanda,
Mikanda imebakia, kula  bada na mlenda,
Na Unguja yamedanda, ya urojo kuusunda,
Wote walionipenda, shukurani nazitoa !

No comments: