Thursday, December 13, 2012

HIVI SASA ASINZIA


Kitu hajakiongea, naona anikoromea,
Hakuna cha kuambua, ila gia za kukataa,
Masikio yaumia, pumziko latakiwa,
Hivi sasa asinzia, mimi naenda kulala!

Wakataa makataa, utumwa kununuliwa,
Viroja wavihofia, na njia wasizojua,
Mafagio wanunua, barabara kufagia,
Hivi sasa asinzia, mimi naenda kulala!

Weupe waliokuwa, kichwani  wameishiwa,
Wabaki kushangilia, hawajui ya kuzua,
Siku ikijawadaia, wasiache kuzubaa,
Hivi sasa asinzia, mimi naenda kulala!

Hili halijawa ngekewa, ni mtego mwategewa,
Nao wanaosinzia, ndoano mmepatiwa,
Na nyavu zinawajia, wapate wengi kuvua,
Hivi sasa asinzia, mimi naenda kulala!

Mnafiki angalia, alama zimemjaa,
Kweli wongo kwake huwa, na ahadi hufulia,
Mwingi wa kuiisifia, hata akitindikiwa,
Hivi sasa asinzia, mimi naenda kulala!

Ishara ukizjua, yake utayaelewa,
Si muhali kujinasua, bora ukaangalia,
Sio rahisi dunia, miteremko ikawa,
Hivi sasa asinzia, mimi naenda kulala!

Hapa ninamalizia, kesho kutoihofia,
Yumkini kukimbia, hakika usiyojua,
Yakini kupalilia, bora litakalokuwa,
Hivi sasa asinzia, mimi naenda kulala!

No comments: