Thursday, December 13, 2012

Hakuna mkamilifu


WAJA hatukujaliwa, ukamilifu kupewa,
Kiasi tunapungua, na wengi tunajijua,
Kadari hatukupewa, ya kuweza kutimia,
Hakuna mkamilifu, hata awe mchamungu!


Mjua mwenye kujua, sababu zake ajua,
Upungufu kutegea, kisa chake akijua,
Ukamili kabakia, kuhodhi mwenye kutoa,
Hakuna mkamilifu, hata awe mchamungu!

Tusije kujihadaa, vingine tukadhania,
Wapambe waliokuwa, miungu kutuumbia,
Wasifu anatakiwa, Mola asiyezaliwa,
Hakuna mkamilifu, hata awe mchamungu!

Viumbe  hatukupewa, ruhusa kujiumbua,
Kwa kelele na kuzua, yale tusiyojaliwa,
Kuridhika ndiyo njia, na kikomo kukijua,
Hakuna mkamilifu, hata awe mchamungu!

Mwanzo wetu twaujua, ila mwisho twaotea,
Uchamungu kiingia, nalo tutakadiria,
Hapa si watu wa kukaa, hii njia  twatumia,
Hakuna mkamilifu, hata awe mchamungu!

Kwa kitambo kulijua, tutaiacha dunia,
Visa tungevipangua, na hoja kujijengea,
Hakuna wa kubakia, usawa tungenuia,
Hakuna mkamilifu, hata awe mchamungu!

Haki tungeangalia, tusende mbele kulia,
Na dhuluma kupungua, moto kutokuumbua,
Na adili kutufaa, mizani ikatimia,
Hakuna mkamilifu, hata awe mchamungu!

Fukara tungewafaa, na wala si kuulea,
Tungepiga vita njaa, na sio kuitumia,
Watu tukawanua, na mfukoni kutia,
Hakuna mkamilifu, hata awe mchamungu!

Tungelijua masaa, huwa ni yetu dunia,
Na fumba na kufumbua, hapa tunaezuliwa,
Isingekuwa ridhaa, uongo kupalilia,
Hakuna mkamilifu, hata awe mchamungu!

Umma tusingeuubia, na ufukara kuutia,
Udhibiti tungetia, haramu kuikataa,
Halali tukailea, h adi mwisho wa dunia,
Hakuna mkamilifu, hata awe mchamungu!


No comments: