Wednesday, January 9, 2013

Mpenzi nimtakaye

 
Ni yule anijuaye, pasi kusema na yeye,
Na wala nisilitowe, awe aitikiaye,
Fikira zzangu zi naye, na zake yeye ninaye,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Ulimbowe si mwiliwe, ila  yake akiliye,
Mambo nizungumzaye, awe anielewaye,
Changamoto atoaye, ubora nisipunguwe,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Hali aielewaye, pasina kupiga yowe,
Dhiki avumiliaye, hata pale nimfinyawe,
Sio siri atoaye, hadi nje zifikie,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Mpenzi nimpendaye, ni yule ayeyukaye,
Ni laini akuwaye, siagi ni mithiliye,
Juani asibakiye, kote atiririkaye,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Mpenzi nimpandaye, si akakamaaye,
Hasira zisimwishiye, mwishowe avunjikaye,
Balaa impataye, awe achanganyikiwaye,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Si anung'unikaye, na mimi nisisikie,
Ni dhahiri aliaye, limuumizalo nijue,
Nami nimsikiaye, na tatizo nitatue,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Mpenzi nimtakaye, ni yule nimtekenyae,
Saa zote achekeaye, hadi machozi atoe,
Kisha aniangalie, awe siye ashibaye,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Mpenzi nimpendaye, si kitu afichaye,
Yangu huwa yake yeye, na yake ni yangu miye,
Si anishtukizaye, matatizoni niishie,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Mpenzi nimakaye, ni yule aningojaye,
Subira asiishiwe, hadi manane ningie,
Mlango afunguaye, tabasamu linivae,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Si yule aamuaye, kwanza ni aulizaye,
Ukweli atafutae, si ya nje asikiaye,
Kisha nasi tuongee, tusilojua tujue,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Ni ukweli asemaye, uongo asiapiye,
Na hofu imjaaye, Mola asimghadhabikie,
Na kesho aigopaaye,  kiama kisimuumbue,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Mpenzi nimpendaye, huwa anidekezaye,
Machozi anifutaye, kwa laini mkonowe,
Kisha anibembelezaye, usingizi unijie,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Mpenzi nimpendaye, ni tunu nijaliwaye,
Kwa juu atokeaye, baraka ajaliwae,
Rehema anileteaye, heri nisipungukiwe,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Mpenzi nimpendaye, ni ahadi atunzaye,
Nadhiri atimizaye, kwa wakati 'sikawie,
Na hali aijuaye, ahadi asiitoe,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Huwa deni alipaye, mpenzi nimpendaye,
Si watu awarushaye, awe aaapiziwaye,
Kizazi yawafikie, hali hili wasijue,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Mpenzi nimtakaye, ni Mola anigaiye,
Si wa shetani nipewaye, pabaya aingizaye,
Majuto ayaletaye, dunia uichukie,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
Mpenzi nimpendaye, ni sababu nijaaye,
Kwanini nimpendaye, ila kubwa kuwa yeye,
Na kisha ni hai niwaye, kila nikiwapo naye,
Mpenzi nimtakaye, ni anijuliaye !
 
 

No comments: