Machoye ya samawati, na nywele ni za
dhahabu,
Kanipiga kwa manati, hadi nimekuwa bubu,
Sumakuye haisiti, yavuta kama kulabu,
Binti wa Kimarekani, akili anichanganya!
Kanimaliza binati, hali yangu taabani,
Ninakuwa kama chizi, kama yeye simuoni,
Chini siwezi kuketi, hadi nimtie machoni,
Binti wa Kimarekani, akili anichanganya!
Kwangu kawa kama kiti, mkweizi wa maruwani,
Simhofu afriti, yeye kinga wa imani,
Nafsi aidhibiti, kingine sikitamani,
Binti wa Kimarekani, akili anichanganya!
Napenda hostelini, avipangavyo vya ndani,
Kwangu ikawa ni shani, kama vile bustani,
Na harufu utadhani, anacuhoma ubani,
Binti wa Kimarekani, akili anichanganya!
Ninampenda kichwani, nywele akizibaini,
Zinazokuja usoni, akarudisha uwani,
Kisha akawa makini, kuteta anachoamini,
Binti wa Kimarekani, akili anichanganya!
Napenda mgahawani, kwa anavyojiamini,
Mkiwa mazungumzoni, watu wakamuamini,
Alama wakazighani, ugavana atawini,
Binti wa Kimarekani, akili anichanganya!
Nampenda darasani, kwa kuwa ni namba wani,
Asiyejali ya nani, akikaa ubavuni,
Hazihofu shotigani, na sheria mkononi,
Binti wa Kimarekani, akili anichanganya!
Mwana huyu mahluti, weusi sio yakini,
Na weupe si wa dhati, unaishia njiani,
Utadhani kalkiti, nyweleze kwa ulaini,
Binti wa Kimarekani, akili anichanganya!
Macho yake ya kijani, huionyesha hisani,
Yakilegea laini, kama nyepesi jibini,
Akilia hujilani, kwa nini umemuhini,
Binti wa Kimarekani, akili anichanganya
Sautiye ya puani, hukutoa mashakani,
Kuisikia ya thamani, ni muziki wenye
shani,
Hauuchoki yakini ,kuisikia hewani,
Binti wa Kimarekani, akili anichanganya
Jina lake Carolyn, anatokea Brooklyn,
Amenipa anwani, nimtafute mjini,
Nikiwasili mwakani, kuiona Marekani,
Binti wa Kimarekani, akili anichanganya