Wednesday, January 16, 2013

Ufisadi ukizidi


Ukizidi ufisadi, kaidi hawafaidi,

Ni sawa na kuritadi, sudi kuuza kwa tadi,

Ikawa ni maabadi, pasina siku idadi,

Ufisadi ukizidi, zuri hugeuka ovu !

 

Uoza pasina udi, harufu mbaya ni jadi,

Maisha yetu abadi, mvuje hauwi waridi,

Na laini si muradi, ikaja kuwa hadidi,

Ufisadi ukizidi, tamu huwa na ugwandu !

 

Hafaidi mkaidi,ila vumbi la magadi,

Msingi bila nakidi, aushi hutaradadi,

Kwako awaye gaidi, kwa mwingine ni shadidi,

Ufisadi ukizidi, heri hugeuka shari!

 

Kwa ubaya akinadi, kwako huwa maridadi,

Dunia alimradi, pepo zake za kunadi,

Na kula mwenye mradi, upandewe hufaidi,

Ufisadi ukizidi, haramu huwa halali!

 

Asiliye maabadi, hadi tulipoinadi,

Kugeuka makuwadi, na wengine mafasidi,

Ikawa yataradadi, na ibada kukaidi,

Ufisadi ukizidi, zuri hugeuka ovu !

 

Ngurumo hizi za radi, umeme na makusudi,

Na kila mleta ulodi,  binafsi anahidi,

Hapana kweli mihadi, isipokuwa ahadi,

Ufisadi ukizidi, tamu huwa na ugwandu !

 

Kila mmaliza kodi, muumiani kazidi,

Mtafutie shahidi, umshushie gredi,

Na kula inapobidi, dawa yake uhasidi,

Ufisadi ukizidi, heri hugeuka shari!

 

Fidadi hana marudi, huzisifia juhudi,

Ya kheri akakaidi, azoze huna bidii,

Akaikosa hamadi, kwa ajali za uradi,

Ufisadi ukizidi, haramu huwa halali!

 

Maradhi huwa yarudi, na afya ikakaidi,

Huwa yaodnoka sudi, ukabaki ugaidi,

Alipokuwa ahadi, ibakie ya fasidi,

Ufisadi ukizidi, haramu huwa halali!

 

Jasmini na waridhi, hukauka kwa kunadi,

Bustani maridadi, ikawa ni murtadi,

Yawe kiza maabadi, shetani yamsujudi,

Ufisadi ukizidi, haramu huwa halali!

No comments: