Sijui
kilichokuwa, wala lililotokea,
Lengo
sikukusudia, na shabaha haikuwa,
Naona
kusalimia, na sio kusalimiwa,
Mkono
nilinyanyua, wewe hukuangalia!
Tumekuwa
ni sanaa, kucheka na kuchekua,
Na
kisha wanaolia, sinema wakafanziwa,
Huruma
sijaijua, ila ujinga kupewa,
Mkono
nilinyanyua, wewe hukuangalia!
Naishangaa
dunia, upuzi ilivyokuwa,
Kile
cha kuwajalia, ndio kinadharauliwa,
Na
hasara kilokuwa, ndio kinathaminiwa,
Mkono
nilinyanyua, wewe hukuangalia!
Njia
niliichagua, sisi sote kutembea,
Nyuma
wewe ukakaa, kama unanitegea,
Njiapanda
kufikia, kushoto ukaingia,
Mkono
nilinyanyua, wewe hukuangalia!
Kamwe
sikukuambaa, unyayo nikafatia,
Nilipokushuhudia,
sikuacha kujitoa,
Kama
ungeangalia, sura usingekosea,
Mkono
nilinyanyua, wewe hukuangalia!
Ukubwa
umekuoa, nasaba kuikataa,
Na
marafiki wakiwa, hutaki kuwasikia,
Juu
umejinyanyua, daraja kujitwalia,
Mkono
nilinyanyua, wewe hukuangalia!
Sitaki
kukuvamia, wala kukukaribia,
Ila
ninashtakia, zamani ilivyokuwa,
Halali
kama ni sawa, Mola atakujalia,
Mkono
nilinyanyua, wewe hukuangalia!
Chako
sijakililia, wala ombaomba kuwa,
Uhusiano
wa riha, sasa nimeutambua,
Ami
hawajatokea, wa kweli waliokuwa,
Mkono
nilinyanyua, wewe hukuangalia!
No comments:
Post a Comment