Monday, January 28, 2013

Yamo Kwenye Mashairi...

Mengi yamehadithiwa, na mifano kutolewa,

Vipande vya historia, darasa mkajaliwa,

Ni vito vilivyokuwa, kinyesini vyafukiwa,

Yamo kwenye mashairi, ila nani anasoma ?

Akili waliojaa, viini wajimwagia,

Kubaini wafulia, sio waliochaguliwa,

Neema ya kubabia, huishi kuiogea,

Yamo kwenye mashairi, nani wa kutafakari ?

Maandishi hutokea, bali hutojisomea,

Akili zikakwambia, wewe sana unajua,

Hadi unakoelekea, njia zako kufungiwa,

Yamo kwenye mashairi, ila nani anasoma ?

Ulidhani wasikiwa, watu viziwi wakawa,

Ulidhani wayajua, ukakuta hayakuwa,

Bishara zikakwambia, njia umeshapotea,

Yamo kwenye mashairi, nani wa kutafakari ?

Zama zilizoishia, mawazo yalifukiwa,

Leo yanachimbuliwa, mengi watu wanajua,

Vitendo wakumbukia, awali vilivyokuwa,

Yamo kwenye mashairi, ila nani anasoma ?

Mizani waichukua, kisha wakaangalia,

Kama sawa imekuwa, au vitu imetiwa,

Kila inapopwelea, kelele utasikia,

Yamo kwenye mashairi, nani wa kutafakari ?

Maji yamewazidia, waogopa angamia,

Bahari nchi kavu kuwa,kwao taabu itakuwa,

Bado hawajatembea, majini wakaelea,

Yamo kwenye mashairi, ila nani anasoma ?

Neema zimesambaa, ja senene na mvua,

Yawashinda magunia, wapi kwingine kukaa,

Na kumbikumbi wazaa, si muda watatokea,

Yamo kwenye mashairi, nani wa kutafakari ?

Isije kuwa balaa, ikawa  kizaazaa,

Kasi itapopungua, mwendo rudi nyuma ukawa,

Na ari ikaishia, moshini kuyoyomea,

Yamo kwenye mashairi, ila nani anasoma ?

Tabia naihofia, dhrau iliyojaa,

Hoja inayonyanyapaa, bila asili kujua,

Mioyo kukangamaa, kama kaukau zikawa,

Yamo kwenye mashairi, nani wa kutafakari ?

No comments: