Monday, January 21, 2013

MTANI: Eti tumeendelea... au tunataniana ?




Hebu muogope Mungu
Nafsi yako uiangalie
Uadilifu sio bidhaa,
Na ukweli hauuzwi sokoni
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Iko wapi sindano
Itokayo Tanzania?

Isiwe ni njaa ya kura
Na kiu cha utendaji
Chaanza kukushambulia
Ndio midia unazivamia
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Iko wapi hiyo pasi
Katengeneza Mtanzania?

Sisi watu wa kununua
Na kisha kwenda kutumia
Kigezo kingelikuwa
Si kwendelea ni kusaidiwa:
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Iko wapi pampu ya maji
Kutokea Chuo Kikuu mlimani ?

Yeyote anayetawala
Na kodi akazisimamia
Mapato yote kuingia
Makubwa atajifanyia
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Liko wapi jambo jipya
Si wajibu kuzungumzia ?

Kuongoza ukichaguliwa
Ni kazi kama kuajiriwa
Kuna mambo unatakiwa
Budi hayo yote kutimia
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Umejenga barabara
Mshahara si umelipwa?

Malipo ukipokea
Na kazi isipotimia
Kabdarasi sawa utakuwa
Cha bure umekipokea
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
LIko wapi trekta letu
Wanauliza wakulima ?

Kaangalie Korea na Malaysia
Hata jamaa wa China na India
Huko huko tumeanzia
Sisi nyuma bado twabakia
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Liko wapi gari lal Nyumbu
Limekufa na Nyerere ?

Vijijini twajionea
Ghorofa zinainukia
Ila si aushi zilizokuwa
Za udongo na nyasi ndio paa
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Vijijini nyumba zikiota:
Hapo kweli tutaendelea ?

Umeme kwetu kumi asilimia
Ishirini itakuwa ikiwa mia
Kwa spidi ya luku kutumia
Na wateja  kudharauliwa
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Gizani tusingelikuwa
Vijijini Tanzania ?

UKosefu bado yetu lugha,
Madawati mashuleni kupotea
Watoto chini wanaokaa
Makalio wakayachubua
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Madawati yatushinda
Eti tumeendelea ?

Vyoo kwetu ni udhia
Bahati ukiviambulia
Visafi  tena vilivyokuwa
Hata vinapochafuliwa
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Kuwa hata nacho hicho choo
Kwa wengi ni mtihani
Eti tumeendelea ?

Uzuri wa wanawake vijijini
Tunazidi kuufanya duni
Haki za binadamu wakowapi
Vijijini wanawauliza
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Dhiki, shida vijijini
Wazuri hawaonekani ?

Maji hadithi inayosifiwa
Alfu lela ulela imekua,
Elfu zimekwishatufikia
Elfu kumi tunazingojea
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Maji kuwa kama almasi
Eti tumeendelea ?

Huwezi ukajisifia
Kwa kile kisichotokea
Au kile kinachokuwa
Na watu wakajionea
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Kuendelea kwa tivii
Hayo maendeleo bandia ?

Wabaya wakizaliwa
Siri yao wanaitambua
Nao wanaweza kujisifia,
Na mapambo kujitia
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Kibaya kawaye ni kujitembeza
Kizuri hadhiye kujiuza!

Kale nilikwishawaambia
Maendeleo ya nchi kufafanua
Yataka watu kujitambua
Wengi chini yanawaondoa
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Wengi palepale wakiwa
Mnaweza kuendelea ?

Sera sasa zinazotakiwa
Ni la wengi kuwa na manfufaa
Ukija kulinyanyua pazia
Watu wote watajionea
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Uongozi kalasi vijijini
Itaendelea Tanzania?

Pesa sasa mnazichukua
Vyombo vya habari kumwagia
Hivi mmekwishatembelea,
Huko kulikokuwa na njaa
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Mjini wanazidi kushiba
Vijijini utapiamlo
Hayo ni maendeleo ?

Wanasiasa waliokuwa,
Nani kijijini anayekaaa
Ila fisadi waliojijengea
Makasiri ya maendeleo kuua ?
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Wako wapi viongozi
Wafanyao kazi vijijini?

Tunaifanya sanaa
Dhana hii ya kuendelea
Si upepo inayozawadiwa
Kisha bendera ikapepea
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Vijiji visipoendelea
Haiendelei Tanzania?

Vya msingi vinatakiwa
Na vingine siye kujinyima
Watu wakishajipatia
Tuongeee kuendelea
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Iko wapi sindano
Itokayo Tanzania?

Aibu tunaojitia
Kwa ukweli kuukataa
Kunayo ndogo kweli hatua
Ila bado kabisa hatujaendelea
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Uongo kurudi nyuma
Maendeleo ni ukweli

Haki ndani inapoingia
Watu wote wakajisikia
Na nchi wakajivunia
Na sio laana wanaozitoa
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Haki isipokuwako
Nani ataendelea?

Sheria zinapochezewa
Na wengine juu yake kuwa
Pakakosekana usawa
Katiba uliyokwiharidhia
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Bila sauti ya wananchi
Maendeleo sio 'mirage'?

Wote kama watoto tukiwa,
Nyumbani kwa baba na mama twakaa
Kulishwa tunategemea
Na wala sio wa kujitegemea
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Uhuru wa kiuchumi
Sio mwanzo wa maendeleo?

Vingine inapokuwa
Watu mashaka tutawatia
Akili wakaziwazia
kama sawa zilizokuwa
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Hili tusipoliangalia
Ukichaa huwa kuendelea!

Moja la kulizingatia
Hususan kwa wote Watanzania
Si watu wanaotuletea
Maendeleo wakajisifia
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Maendeleo kodi yetu
Kama isipofisadiwa ?

Siasa zilikoingia
Kila kitu zinakichafua
Hata akili waliokuwa
Nao sasa wazainiwa
Ukweli kuukataaa
Mbeleko ya uongo kubeba:
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Mswahili ninavyomjua
Ukimwambia ameendelea:
Hapo hapo huishia!


Nayakumbuka ya bibiyangu
Daa zamani alipoiingia
Shogaye akamuelezea
Analo shamba lake hilo kubwaaaaaaa...
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Robo eka wala  haikufikia
Wa pwani amekwishaendelea!

Naona ndio tuliojaliwa
Kwa sifa ninazozisikia
Hakuna tena kilichobakia
Ila sasa tuanze kuvitumia:
Ewe babu, ewe bibi
Ewe baba, ewe mama
Ewe kaka, ewe dada
Kaulizie kigezo tumikishi:
Tanzania tumelima robo eka:
Malaysia 'hekta' za kwao ni mia moja:
Ni nani wa kujisifia?

No comments: