Saturday, January 26, 2013

Uchina kasomesheni

Dunia inaegema, mashariki kuhamia,

Ndiko kuliko neema, na salama kujaliwa,

Mzazi aliye mwema, mwana atamwambia,

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

Wanaolea dhuluma, yawakimbia dunia,

Kwingineko wamehama, Afrika kuhamia,

Maisha yao nakama, na watu kuvurugia,

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

Mchina awapa homa, hawakai wakakaa,

Wanakiona kiama, si mbali kinaajia,

Afrika kuigema, ndiyo kubwa yao nia,

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

Wamezoea kuchuma, kwa wengine kuibia,

Maziwa wanayokama, kutoka yanakataa,

Matumbo yawanguruma, wapi kwenda kuhamia,

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

Maisha yao daima, kwa wengine kwenda vua,

Hawajali yako hima, nuksi hukuachia,

Wa kwako wakaroroma, na silaha kuzikwea,

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

Maisha yao hujuma, na msaada udhia,

Vipi wewe mtu mzima, lawalawa wapokea,

Mgodi ukautema, bakshishi kupokea?

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

Busara zimetuhama, ni watu wa kubabia,

Twadharau wetu umma, wageni watuzuzua,

Kigingi ni mkulima, mnunuzi hatokaa,

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

Imepotea hekima, kwa ukubwa kulilia,

Hapo tulipoegema, mbona mengi tumepwaya,

Hii ya ovyo kalima, lazima kuumbuliwa,

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

Wewe baba, wewe mama, Zatakiwa njia mpya,

Kituo cha kusimama, kuanzia Malaysia,

Indonesia nako hima, panafaa kuchungua,

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

Za wazungu ni gharama, sasa zitatuumbua,

Rushwa kuwa mlima, tushinde kujipandia,

Twendeni kwenye neema, kwenye njaa kukimbia,

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

Wakwezi ninawatuma, wengine kuwaambia,

Hususan Wakulima,Morogoro walokaa,

Halafu ninawatuma, wafugaji kuwaambia,

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

Nchi yataka neema, na elimu kuenea,

Ikipungua gharama, wengi tutafanikiwa,

Na katika hizi zama, ubia unatakiwa,

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

Ubia sasa lazima, na vyuo vya Malayasia,

Akili wakzituma, kuhamia Tanzania,

Na matawi kuyafuma, urahisi kwetu kuwa,

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

Ubia kitu cha hima, na Wachina kuingia,

Vyuo kwao vikahama, kuhamia Tanzania,

Mitandao ikafuma, ubora sawa ukawa,

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

Ninamuomba Rahima, macho kuja tufungua,

Tukaipata neema, sana tunayoililia,

Zigeuke zetu zama, kwa nafuu kuingia,

Uchina kasomesheni, kwa nafuu na salama !

No comments: