Tuesday, January 29, 2013

Hanky -yo, bado ninayo

CHA mkonokitambaa, machozi ulofutia,

Mimi nilikichukua, na sasa nakitumia,

Machozi kujiuftia, kwa wewe kuondokewa,

Hanky -yo, bado ninayo, najifutia machozi!

Marashiyo yanukia, kama vile yanalia,

Na poda uliyotia, kikohozi yanitia,

Kila nikijiwazia, kosa langu sijajua,

Hanky -yo, bado ninayo, najifutia machozi!

Ufukara nakisia, waweza ukachangia,

Njaa ninayonukia, rahisi kuifichua,

Wewe ulipogundua, hukuweza vumilia,

Hanky -yo, bado ninayo, najifutia machozi!

Kwaheri hukuitoa, wala kunisimbulia,

Njia uliichagua, ifaayo kufatia,

Upweke kuniachia, mwenye nacho kujaliwa,

Hanky -yo, bado ninayo, najifutia machozi!

Ila ninachokijua, langu kweli lilikuwa,

Mizanini ungetia, zana ingelizubaa,

Kwa upande kuzidiwa, hadi chini kugotea,

Hanky -yo, bado ninayo, najifutia machozi!

Moyo nilikuachia, upate kupalilia,

Bustani kuchanua, mengine yangefatia,

Haraka uliyokuwa, hukuweza jizuia,

Hanky -yo, bado ninayo, najifutia machozi!

Kuishi ulihilakiwa, mapema kutangulia,

Fisadi kumkimbilia, idadi asiyewajua,

Silaani, ninakwambia, hilo utalijutia,

Hanky -yo, bado ninayo, najifutia machozi!

Ya kweli umeachia, ukafata ya kuzua,

Yaliyojaa sanaa, ukweli zisizokuwa,

Laiti ningelijua, nisingelikuangalia,

Hanky -yo, bado ninayo, najifutia machozi!

Laiti ningelijua, nisingelikuangalia,

Machowe yalolegea, ukawa wanilogea,

Nami sikujitambua, na ukweli kuujua,

Hanky -yo, bado ninayo, najifutia machozi!

No comments: