Kushoto umeptia, kulia ungegeukia,
Hali ukaitambua, na vyanzo kuvielewa,
Haraka ukitumia, mguu utaumia,
Watu wakishaamka, wape kazi wakafanze !
Watu wajiamkia, maji ni kuwapatia,
Uso wapate kunawa, tongotongo kuondoa,
Na njia ya kufungua, kwanza kuwasalimia,
Watu wakishaamka, unawapa blanketi ?
Vitisho wamezoea, tangia ya kuzaliwa,
Hadi mamba watumiwa, na simba akafatia,
Hofu walishaivua, hasira imebakia,
Watu wakishaamka, wape kazi wakafanze !
Jua wanajionea, chiniye yanayotokea,
Giza wala halijawa, vipi unafikiria,
Na hesabuu wazijua, waweza kukutajia,
Watu wakishaamka, unawapa blanketi ?
Staftahi wangojea, weye wawakoromea,
Na mgeni alokuwa, siye wao, wakujua,
Heshima ukikosea, nani nguo ajivua ?
Watu wakishaamka, wape kazi wakafanze !
Sheria hujadumaa, haki isipoijua,
Dhuluma ikandaiwa, na mengi kusingiziwa,
Na mikuki kutupiwa, kila inapotokea,
Watu wakishaamka, unawapa blanketi ?
Kuteta ni kufikiria, wala si jambo kuzua,
Neno lisipoangaliwa, vita laweza kuzua,
Haki ikibaguliwa, huja ngao ikavaa,
Watu wakishaamka, wape kazi wakafanze !
Mambo yataka hatua, nyumbani yakabakia,
Hadharani kutotoa, chunguni yanapokuwa,
Au wote tutakuwa, nasi ni watuhumiwa,
Watu wakishaamka, unawapa blanketi ?
Ugaidi mwanunua, kwa
faida kutumia,
Ya kwenu kujijengea, hali ya umma yapwaya,
Kila mwenye kuyajua, uongo huugundua,
Watu wakishaamka, wape kazi wakafanze !
Yabadilika dunia, kadhalika Tanzania,
Hakuna aliyepewa, hatimilki kutwaa,
Yake kujiamlia, jinsi anavyojisikia,
Watu wakishaamka, unawapa blanketi ?
No comments:
Post a Comment