Monday, January 28, 2013

U M O J A W A K I T A I F A


KAMA hujaligundua, wala siri haijawa,

Kwa tunakoelekea, uhuni wafichuliwa,

Dhahiri inaingia, watu wote kuijua,

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

Ukabila Tanzania, wa chama umebakia,

Na nchi kuiokoa, ni lazima kujifia,

Usawa ukaingia, nafasi kupigania,

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

Koo tutajazigawa, uchama kuendelea,

Na vijiji kufulia, kitu visije ambua,

Uongo tunaozua, haujengi, wabomoa,

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

IJe mbele Tanzania, mengine yakafatia,

Vinginevyo tutalia, nchi tukaililia,

Tanzania, Tanzania, nchi yangu wapotea,

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

Wote tunajitambua, uhai unatufaa,

Wazushi wa kuzuzua, lazima kuwafichua,

Mkao wanaokaa, haunao njema nia,

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

Wengine wanahofiwa, shetani awatumia,

Kichwani keshaingia, mbio awafukuzia,

Ya shari kukimbilia, nchi ije angamia,

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

Nusura tukiijua, vyema tutawachingua,

Sababu na yao nia, ukubwa kuulilia,

Au ikulu inshakuwa, danguro la kuhamia?

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

Waliojaa madoa, na hata likiwa doa,

Ushauri nautoa, ngazi budi kuachia,

Safi tunaodhania, gidamu wakachukua,

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

Haiwi haitakuwa, ubora wa kununua,

Halali ukajitia, na ngazi kujipandia,

Hima haitasalia, nia itakubetua,

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

Mapema naashiria, siri zinafichuliwa,

Mengi tusiyoyajua, mbona sasa twayajua,

Kila mwanzia ubaya, hatima huwa ubaya,

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

Vyama vyetu hujifia, hoja zinapopungua,

Na uchafu kununua, wengine kuwatupia,

Hadhari ninaitoa, hiyo kwetu siyo njia,

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

Wanasiasa mwafaa,  kuikoa Tanzania,

Nafasi mkiachia, mtakuja kuzomewa,

Umoja mngeanzia, wa vyama kupigania,

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

Kisha mkajichungua, bora wenu kuwajua,

Bila ya kufikiria, chama gani atokea,

Nahodha anayefaa, nchi hii kuokoa,

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

Mipaka mkaondoa, kwa adili kuijua,

Na safi kilichokuwa, nchi mkaipatia,

Imani zinatakiwa, kazi hii kutetea,

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

Twataka atayetufaa, na wala sio balaa,

Tunataka manufaa, wala si kuhofia,

Salama ya Tanzania, alo bora kuchagua,

Umoja wa kitaifa, ni vigumu kukwepeka!

 

No comments: