Saturday, January 26, 2013

Pendo lisilochipua


AIMA nitakumbuka, nilizopiga hatua,

Nikitamani kukushika, neno nikakuambia,

Bali nyuma nilivutika, nawe ukatangulia,

Pendo lisilochipua,  moyoni linabakia !

 

Msingi tulipofika, japo nilikutania,

Midomo nikaishika, kupapasa nikajua,

Matokeo yalipotoka, sote hatukwendelea,

Pendo lisilochipua,  moyoni linabakia !

 

Baada tu ya mwaka, nawe ukajaingia,

Mtaa juu ulitoka, wa chini nikaanzia,

Mwendowe nikaudaka, usingizini nikiwa,

Pendo lisilochipua,  moyoni linabakia !

 

Na kila nilipotaka, jambo langu kukwambia,

Ulimi ulifyatuka, salamu tu kuitoa,

Machowe yaliniteka, hadi nguvu kuishiwa,

Pendo lisilochipua,  moyoni linabakia !

 

Miaka ikafutika, umbali ukaingia,

Hadi niliposumbuka, na hadithi kuambiwa,

Dar umebahatika, kazi unajifanyia,

Pendo lisilochipua,  moyoni linabakia !

 

Sikuwa nayo haraka, hadi nilipochelewa,

Na mara nilipofika, mbele ulishatangulia,

Machoni ukanitoka, urulaini kwenda kuwa,

Pendo lisilochipua,  moyoni linabakia !

 

Ajabu haya mashaka, hayakunipa ukiwa,

Bure sikutaabika, zaidi ningelilia,

Letu halikuandikwa, na wala lisingekuwa,

Pendo lisilochipua,  moyoni linabakia !

 

Ila ninayo hakika, moyoni unachanua,

Jinalo siachi tamka, na wengine kugawia,

Mtu akiliitika, naona unarejea,

Pendo lisilochipua,  moyoni linabakia !

 

Hautorudi hakika, hilo ninalitambua,

Ila siku itafika, na mimi nikiingia,

Kwanza nitalolitaka, wapi wakaa kujua,

Pendo lisilochipua,  moyoni linabakia !

 

Kama inaruhusika, wewe nitakuchagua,

Mkono nikakushika, ukirimba kulilia,

Wengine sintowataka, ila wewe maridhia,

Pendo lisilochipua,  moyoni linabakia !

No comments: