Saturday, January 26, 2013

Unataka kusifiwa


Isije sasa ikawa, ndugu umekwishapagawa,

Unataka kuchezewa,  ngoma tusiyoijua,

Na kibwebwe wajitia, uwanjani kuingia ?

Unataka kusifiwa, kwa wajibu kutimiza?

 

Utoto unatutia, kama tusiotambua,

Kile unachotakiwa, kwa ngwee kujilimia,

Twaona inapungua, wewe wzidi tutambia?

Unataka kusifiwa, kwa wajibu kutimiza?

 

Sasa umelichokoa, nasi tunalizomea,

Vigelegele ikiwa, kama havitasinzia,

Ukweli watu wajua, vingine haitakuwa,

Unataka kusifiwa, kwa wajibu kutimiza?

 

Ni nani anayejua, mbali tungeshafikia,

Laiti ingelikuwa, haki imesimamiwa,

Na fisadi kuwaniwa, masomaso kuwatoa,

Unataka kusifiwa, kwa wajibu kutimiza?

 

Tambo ninazishangaa, kwa kazi za kupangiwa,

Na saada la kufaa, nyuma limeshehenea,

Kisha mtu kuwazia, sifa akajipambia,

Unataka kusifiwa, kwa wajibu kutimiza?

 

Kiherehere najua, watu wengi waugua,

Na tivii kutujia, wote tunakimbilia,

Hata wenye sura mbaya, wapenda kumulikiwa,

Unataka kusifiwa, kwa wajibu kutimiza?

 

Hayo ninajionea, nashindwa kuvumilia,

Adili naililia, uongo kuukimbia,

Nchi haitofanikiwa, mbwembwe tukitegemea,

Unataka kusifiwa, kwa wajibu kutimiza?

 

Mapambo yanazidia, na gharama zazidia,

Hesabu ukijakupewa, kijiji kingelipaa,

Kama Ulaya kikawa, pasenti kingelipewa,

Unataka kusifiwa, kwa wajibu kutimiza?

 

Na safari za kuzua, mtu usipotulia,

Wala kazi kuizua, matunda  itayozaa,

Linanizidi butwaa, utani ninajionea,

Unataka kusifiwa, kwa wajibu kutimiza?

 

Mwaweza kunichukia, ukweli sintouua,

Daima nitautoa, chama kilishanambia,

Matapishi kurejea, kula kwangu haijawa,

Unataka kusifiwa, kwa wajibu kutimiza?

 

Ibilisi kaingia, wafuasi achezea,

Ya ovyo tunayazua, chama yasiyosidia,

Aibu tusipojua, kuaibika tabia,

Unataka kusifiwa, kwa wajibu kutimiza?

 

Kila tunalolizua, na sisi tutazuliwa,

Kashfa mbona balaa, makapuni zimejaa,

Muda unasubiriwa, uvundo kuuachia,

Unataka kusifiwa, kwa wajibu kutimiza?

 

Wa mwenzio 'sipomlea, wako hatatengemaa,

Wapi ulijionea, salama linalokuwa,

Shamba lililokaribia, gugu linapoachiwa ?

Unataka kusifiwa, kwa wajibu kutimiza?

 

 

Mharibu cha jamaa, chake kitharibiwa,

Kila mpenda ubaya, ubaya humfatia,

Ila kheri mkimbilia, kheri itamlilia,

Unataka kusifiwa, kwa wajibu kutimiza?

 

No comments: