Wednesday, January 16, 2013

CHANGU ULINYANYAPAA

Changu kilipungukiwa, mbali ukakiambaa,

Wala hukukipitia, hali yake kuijua,

Ikawa kama wajua, kwako hayatatokea,

Changu ulinyanyapaa, kumbe yatakutokea ?

Mizimu ilichukia, kwa uliyoyanuia,

Kisha ikakutegea, pabaya kuangukia,

Somo hukulielewa, wala hutolielewa,

Changu ulinyanyapaa, kumbe yatakutokea ?

Kwa aliyekuchukulia, kama wake ulikuwa,

Wewe ukadhamiria, baki vile amekuwa,

Na wajibu kujitoa, nasaba ukaiavua,

Changu ulinyanyapaa, kumbe yatakutokea ?

Neno wakijisemea, Mungu anawasikia,

Wagonjwa waliokuwa, milango hufunguliwa,

Kalima kukubaliwa, malipo yako kupewa,

Changu ulinyanyapaa, kumbe yatakutokea ?

Laiti ungelijua, cheo usingetumia,

Juu ukajipitia, vya chini kuvichukia,

Udugu ukafumua, na nasaba kupangua,

Changu ulinyanyapaa, kumbe yatakutokea ?

Sasa yanakutokea, kwa uzito yanajaa,

Yaja yameshehenea, na vituko kuingia,

Dhihaka utadhania, mja inakuchezea,

Changu ulinyanyapaa, kumbe yatakutokea ?

Dua usipoijua, ibada kuikataa,

Nyuma kutorudia, wapi ulipoangukia,

Na tawba kufikia, bado shere itakuwa,

Changu ulinyanyapaa, kumbe yatakutokea ?

Nafuu ulishapewa, yako ukakimbilia,

Kuikusanya dunia, mfukoni kuitia,

Ila ninachohofia, yakukusanya dunia,

Changu ulinyanyapaa, kumbe yatakutokea ?

Suluhu ungeijua, amani ungelipew,

Ovyo umeidhania, na dharau kuitia,

Chambo umekichambua, na kitanzi kujitia,

Changu ulinyanyapaa, kumbe yatakutokea ?

Mbele nilitangulia, sio kwa kutojijua,

Mengi nikayaachia, na vichache kuchagua,

Kuna vingi vya dunia, kubeba huwa ukiwa,

Changu ulinyanyapaa, kumbe yatakutokea ?

Na hasa papa ukiwa, ukadhulumu dagaa,

Hatua itafikia, wenzi kukugeukia,

Ukajikuta mkiwa, huna cha kutumainia,

Changu ulinyanyapaa, kumbe yatakutokea ?

No comments: