LIMEZUKA jinamizi, ardhi haiwahifadhi,
Wauliza waulizi, utadhania bazazi,
Maswali yao yaudhi, yashika kwenye mizizi,
Amfichiaye mwizi, hivi naye sio mwizi?
Lingine hawaulizi, wauliza ufichizi,
Mhifadhi vya waizi, hivi naye sio mwizi?
Wauma vichwa wajuzi, jibule hawaliwezi,
Amfichiaye mwizi, hivi naye sio mwizi?
Kikali kigugumizi, meno yakauma fizi,
Na tabasamu la ndizi, linageuka kiazi,
Wakawateta wakwezi, pia na wapiga mbizi,
Amfichiaye mwizi, hivi naye sio mwizi?
Wawapaa usingizi, vitanda hawaviwezi,
Tivii zawa machizi, kwa kugoma ving'amuzi,
Hakuna kilo azizi, tuhuma haziwalazi,
Amfichiaye mwizi, hivi naye sio mwizi?
Vinara wa mafichizi, na gwiji wa ufukizi,
Mbio wanazidarizi, kuyageuza Uswizi,
Na huku zatamba radhi, za wanyonge kwa
walozi,
Amfichiaye mwizi, hivi naye sio mwizi?
Yamegota mapinduzi, pamebaki siyawezi,
Na ziada vidokozi, kama nusu jambawazi,
Yaliyojiri majuzi, ndio kisa manukuzi,
Amfichiaye mwizi, hivi naye sio mwizi?
Hapanao ugunduzi, uhujumu uko wazi,
Sahani sio saizi, unazidi upotezi,
Watumia nne nazi, hali moja inakidhi?
Amfichiaye mwizi, hivi naye sio mwizi?
Yanawafika wazazi, wa ufu utandawazi,
Kwa kujifanya wajuzi, wa kuyachoma
mandazi,
Kukaanga hawawezi, jadi yao haifunzi,
Amfichiaye mwizi, hivi naye sio mwizi?
Wamuhofuo Mwenyezi, dalili zake ni wazi,
Mbingu na yote ardhi, kaifanzia malezi,
Ayafanyaye maudhi, haipati yake radhi,
Amfichiaye mwizi, hivi naye sio mwizi?
No comments:
Post a Comment