Tuesday, January 29, 2013

DNA Gaidi


HUYU mkubwa gaidi, lazima kumwangamiza,

Atufanyia ukaidi, ndoa zetu kuziponza,

Ili yeye afaida, asichokipandikiza,

DNA gaidi, anapaswa kuuawa!

 

Marikani kamkodi, kuja kutukengeuza,

Kama vichaa twanadi, dokta tutamueleza,

Yamekuwa maabudi, twasali bila tawaza,

DNA gaidi, anapaswa kuuawa!

 

Wenza wapanda midadi, watoto kuwakataa,

Wenye sura za kifodi, uzuri unawakwaza,

Na Jaluo wananadi, weupe kwao muujiza,

DNA gaidi, anapaswa kuuawa!

 

Walala kifudifudi, malengo kuyapoteza,

Uchawi huu wa lodi, mweusi hatauweza,

Ni mkubwa ugaidi, Mzungu tu atauweza,

DNA gaidi, anapaswa kuuawa!

 

Yakija bila magadi, waweza kuyapuuza,

lla halina ahadi, lenyewe linajitweza,

Huzuzuka likibidi, maneno likateleza,

DNA gaidi, anapaswa kuuawa!

 

Kamtazame Daudi,  jinsi anavyowaza,

Imani imekaidi, na hisia zamponza,

Anajiona kafidi, dharau inamkwaza,

DNA gaidi, anapaswa kuuawa!

 

Gaidi kwa umaridadi, ulimbo auuguza,

Watu wasipojirudi, nyumba hatutaziweza,

Ikajapaa idadi, za wazazi wa pwekeza,

DNA gaidi, anapaswa kuuawa!

 

Kesi hii murtadi, yenyewe yajieleza,

Haitaki mashahidi, hakuna wa kuibeza,

Inajiona shadidi, kila kazi yatimiza,

DNA gaidi, anapaswa kuuawa!

 

Imezishusha gredi, ndoa zilizo aziza,

Watu walizokindadi, na wana wa miujiza,

Hadimu kuwa hadidi, dunia yajitangaza,

DNA gaidi, anapaswa kuuawa!

 

Zinayoyomea sudi, za uzazi uso viza,

Wachafuka ukuwadi, na wana wa kuagiza,

Atunusuru Wadudi, huko mbele kuna giza,

DNA gaidi, anapaswa kuuawa!

No comments: