Saturday, January 26, 2013

Hiyo ndio siri yangu

Hainitezi dunia, yake nikakimbilia,
Ni kiboko wa hadaa, ilipo huifichua,
Ujinga hatukuzawa, na kwao hatukuumbiwa,
Hadaa naikataa, hiyo ndiyo siri yangu !
 
Siku unakaribia, mafuta kujiondoa,
Juu kuja kuelewa, maji chini kubakia,
Kweli itapoingia, na uongo kujitoa,
Uongo katu sipendi, hiyo ndiyo siri yangu!
 
Siku inakaribia, mjinga kujielwa,
Werevu ukazaliwa, na hoja zikatolewa,
Wajanja wasiojua, aibu kuwaingia,
Umbeya naukimbia, hiyo ndiyo siri yangu!
 
Pia nao wa kuzua, hesabu wahesabiwa,
Namba ikishafikia, yote moja itakuwa,
Hapana la kujaliwa, ni ukweli kurejea,
Shiriki siikubali, hiyo ndiyo siri yangu!
 
Na wanaomswalia, shetani pasi kujua,
Wito watausikia, roho zikawagutuwa,
Ubaya wakaujua, na talaka kuitoa,
Wema hakika ni jadi, hiyo ndiyo siri yangu!
 
Mitego wataijua, izukapo adilia,
Ukweli ikafichua, hekalu kutengemaa,
Shetani atapolia, na uchi akajijua,
Fitina huwa sitaki, hiyo ndiyo siri yangu!
 
Si nabii wa kuvaa, majoho yasiyokuwa,
Kwa kuifata hadaa, na vitimbi vya dunia,
Na utume sikupewa, zama ulikwishaishia,
Maneno huwa sipendi, hiyo ndiyo siri yangu!
 
Nilipo nimetulia, funguo nazingojea,
Ukiingia wasaa, nije kuwasimulia,
Hakika wa kurejea, visa hawezi kuzua,
Vitendo kwangu ashiki, hiyo ndiyo siri yangu!
 
Nimezitoa hisia, ujumbe kuwafikia,
Haya mkifikiria, mema yanawangojea,
Ila ninachohofia, mtihani kujikomboa,
Kuendeleza wengine, hiyo ndiyo siri yangu.
 
Namshukuru Jalia, kwa dhikiri kuitoa,
Nao waliojaliwa, langu wamelisikia,
Yawangojea hatua, daraja kuifikia,
Kuridhika na kadari, hiyo ndiyo siri yangu!

No comments: