HAYA kinagaubaga, nasema mazagazaga,
Hauwezi kunizuga, vingine ukanitega,
Hilo litakuwa soga, vigumu mimi kumega,
Mamboyo mazagazaga, hebu acha kunikoga.
Mengine mkiyaiga, wenyewe mnajiroga,
Wenzene watia sega, nyie vitako vyagomba,
Wao wajua kutaga, nyie mwajua kuaga?
Mamboyo mazagazaga, hebu acha kunikoga.
Utadhani wakufuga, wakakuvalia njuga,
Kisha kutabananga, kwa teule nazo soga,
Mwana bin kuvuruga, mzaliwa rugaruga,
Mamboyo mazagazaga, hebu acha kunikoga.
Toka lini naye Mchagga, akawa ndonya
atoga,
Mmakonde kutobiringa, na mbega akaiswaga,
Watu wasimwite mwanga, na kelele kuzipiga,
Mamboyo mazagazaga, hebu acha kunikoga.
Iga we mwana wa kuiga, tembo hufa kwa
kiboga,
Ukitingisha mabega,hio wala si kuringa,
Na kila lenye kunoga, wahuni
hulivuruga,
Enzi zao Viburugwa, washamba kwenda
kukoga,
Manyanga weshayabwaga, wabakia kujizuga,
Ngebe ikiwa ngariba, yataishia ujuba,
Mamboyo mazagazaga, hebu acha kunikoga.
Maisha sasa kusagwa, na vijinga vya
ujinga,
Nasaba zake kuiga, na tambo za kujiganga,
Husuda kumbe hufugwa, wasiotaga, kutaga,
Mamboyo mazagazaga, hebu acha kunikoga.
Msiba hujavuruga, yaliyopangwa kubwaga,
Mzaramo na mafiga, ngomaye haiitwi mbega,
Kuzika haiwi kinga, ya umbali kuchabanga,
Mamboyo mazagazaga, hebu acha kunikoga.
Mwanamme kama mwoga, mke kinyonga humwiga,
Rangi akazikoroga, mazingira kuenga,
Maisha yenye kuvunga, mwishowe huwa
kupenga,
Mamboyo mazagazaga, hebu acha kunikoga.
Mwanamme bila nanga, chombowe hakina anga,
Kokote chaweza tinga, na ghubani
kikazinga,
Kiumbe mwenye kuringa, kifafa humcharanga,
Mamboyo mazagazaga, hebu acha kunikoga.
Maleenga ukimtenga, adili unazitwanga,
Na akili kuzinyonga, ukauenzi ujinga,
Kiuno pasina shanga, huwa chaisha uchanga?
Mamboyo mazagazaga, hebu acha kunikoga.
Walinikoga Mapinga, shabaha walizolenga,
Kinachowapiga chenga, mitihani kuwaganga,
Mshairi ninalonga, hamba halianisonga,
Mamboyo mazagazaga, hebu acha kunikoga.
Yangu mkiyapinga, yatakuja kujipganga,
Yakachanua kianga, na sambamba kuviringa,
Duara ikijatinga, na rohoni kuviringa,
Mamboyo mazagazaga, hebu acha kunikoga.
No comments:
Post a Comment