Friday, February 10, 2012

Enzi za ubabe mwisho

Katika nchi hakuna, ya mtu hati miliki,
Akawa mweye kunena, na wengine kuafiki,
Tunataka umakini, usawa pia na haki,
Enzi za ubabe mwisho, sasa ni mazungumzo!

Hakuna kuzungushana, na kwa mbinde kuafiki,
Tunapaswa kupashana, dhuluma kuzitaliki,
Na keki tukagawana, pasipo ya uzandiki,
Enzi za ubabe mwisho, sasa ni maelewano!

Hakuna tena ubwana, na binafsi milki,
Twaukataa utwana, kugeuzwa mamluki,
Wajibu kushirikiana, haina fursa hamaki,
Enzi za ubabe mwisho, sasa ni demokrasia!

Watu wataka bayana, uwazi na ushiriki,
Tabia ya kufichana, yakini haistahiki,
Rahisi kuibiana, dola ukishamiliki,
Enzi za ubabe mwisho, sasa ni mazungumzo!

Udikteta hapana, nchini hatuutaki,
Na uchwara kuachana, hapa kwetu wasibaki,
Tumuombe Maulana, jambo hili kuafiki,
Enzi za ubabe mwisho, sasa ni maelewano!

Hartoyataka Haruna, wala naye Mwanabaki,
Nchi kuwa muamana, hawafai wanafiki,
Usiku huwa mchana, nuru ukaifariki,
Enzi za ubabe mwisho, sasa ni demokrasia!

Maelewano amana, watu waache hamaki,
Watu wakisikilizana, kufanza haishindiki,
Kisha kuendelezana, mambo wakayaafiki,
Enzi za ubabe mwisho, sasa ni mazungumzo!

Mazungumzo hazina, mtaji hutamalaki,
Watu wakakusanyana, na kujenga ushiriki,
Nchi ikashikamana, ufakiri kutaliki,
Enzi za ubabe mwisho, sasa ni maelewano!

Udikteta laana, tena ni kubwa hilaki,
Kadhia kuzuiana, muhimu kuliafiki,
Ataenzi Maulana, nchi nayo halaiki,
Enzi za ubabe mwisho, sasa ni demokrasia!

No comments: