Katika miaka hii, ya nazi kufanywa tui,
Adui kuwa akhii, na mlinzi Mmasai,
Na watu wengi laghai, kweli waliokinai,
Haiwezi kuwa hoja, kuzaliwa tumbo moja!
Hai wasokuwa hai, na mui waso na rai,
Wafanyao baibui, kugeuzwa buibui,
Na sinia makarai, wafaao hawafai,
Haiwezi kuwa hoja, kuzaliwa tumbo moja!
Mdaiwa kuwa mdai, na mwenye njaa hajui,
Wajanja magoigoi, na mbumbumbu wasanii,
Uhai ukawa hoi, taabani tandabui,
Haiwezi kuwa hoja, kuzaliwa tumbo moja!
Janibu kuwa jinai, na ghaibu maslahi,
Huzuni ikafurahi, na furaha kuzirai,
Hayaishi majidai, na mafao hayafai,
Haiwezi kuwa hoja, kuzaliwa tumbo moja!
Sijawa mpiga nai, na midundo sitambui,
Ila hili ninarai, wajuao kujiwahi,
Mazazi mengi nishai, upweke siukinai,
Haiwezi kuwa hoja, kuzaliwa tumbo moja!
Friday, February 17, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment